Na. WAF- Geneva, Uswisi
Tanzania imeshiriki Mkutano Mkuu wa 76 wa Nchi Wanachama wa Shirika la Afya Duniani, ulioanza Tarehe 21 hadi 30 Mei 2023 kwa lengo la kufanya maamuzi ya kisera yanayoongoza mikakati na afua mbalimbali katika Sekta ya Afya Duniani.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mhe. Nassoro Ahmed Mazrui ambaye pia ni Kiongozi wa msafara wa viongozi na timu ya wataalam kutoka Tanzania walioshiriki kwenye Mkutano huo kupitia taarifa yake kwa umma juu ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.
“Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni Miaka 75 ya Shirika la Afya Duniani: Okoa Maisha, Wezesha Afya kwa Wote, ikimaanisha kwamba wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likisherehekea miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, watu wote wawe na afya njema na maisha salama.” amesema Mhe. Marzui.
Pia, amesema katika mkutano huo Tanzania inatarajia kufanya mawasilisho mbalimbali pamoja na ajenda za mkutano huu ambapo ujumbe wa Tanzania utakuwa na vipaumbele vya nchi utakaotumia nafasi zilizopo katika mkutano huu ili kupata fursa za uboreshaji wa shughuli za kushughulikia afya za Watanzania.
Aidha, amesema pamoja na mambo mengine makuu Tanzania itawasilisha vipaumbele vyake kadhaa ambavyo ni pamoja na kuimarisha afya ya msingi na kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto.
Lakini pia amesema katika kikao hicho wamejadiliana namna ya kuanzisha viwanda vya ndani vya kutengeneza dawa na vifaa tiba, kuimarisha mifumo ya Tehama katika utoaji wa huduma za afya, udhibiti wa magonjwa ya yasiyoambukiza ikiwemo Kansa, Siko seli, magonjwa ya akili, kisukari, mikakati ya kuweka utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko hasa yenye kutishia usalama wa afya duniani, na huduma za lishe.
“Nchi yetu itaendelea kushirikiana na jamii ya kimataifa pamoja na wadau wengine katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii ya Watanzania hivyo nasisitiza kuwa Serikali yetu ina jukumu la kuokoa maisha na kuwezesha afya kwa kila mmoja wetu kama kauli mbiu ya Mkutano huu inavyosema, “Miaka 75 ya Shirika la Afya Duniani: Okoa Maisha, Wezesha Afya kwa Wote” amesisitiza Mhe. Mazrui
Mhe. Mazrui amesema ameambatana na ujumbe wa viongozi ambao ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Abdalla Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Dkt. Wilson Mahera Charles, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Prof. Tumaini Nagu, Mganga Mkuu wa Serikali pamoja na watendaji mbalimbali wanaoshughulikia masuala ya Afya kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wadau wanaojihusisha na masuala ya Afya.