Mkurugenzi wa uthibiti, ufuatiliaji na tathmini NACTVET, Dk Jofrey Oleke akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha kuhusu udahili huo.
Julieth Laizer,Arusha
Arusha. Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET),limefungua dirisha la udahili huku likivionya vyuo vitakavyoharibu mchakato wa udahili kusitishiwa udahili kwa mwaka huu.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi Uthibiti, Ufuatiliaji na Tathmini wa NACTVET, Dk Jofrey Oleke,wakati akitangaza kuanza kwa udahili kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada, katika kozi zinazotolewa na vyuo mbalimbali nchini kwa mwaka wa masomo 2023/24.
Aidha Dirisha hilo la udahili wa wanafunzi kwa ngazi ya Astashahada na Shahada kwa kozi zinazotolewa na vyuo mbalimbali nchini limefunguliwa leo Jumapili Mei 21 hadi Juni 30,2023 katika awamu ya kwanza .
Dk Oleke amesema endapo kuna chuo kitakiuka masharti ya udahili hawatasita kukichukulia hatua kali kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
“Kabla ya ufunguzi wa udahili,tulikaa na vyuo vyote ambavyo vinahusika na udahili wa wanafunzi katika kada hii ya kati na tukakubaliana na yeyote atakayehusika kuharibu mchakato wa udahili atasitishiwa udahili wa mwaka huu kwa hiyo vyuo vinatahadharishwa kuhakikisha vinazingatia taratibu za udahili kama ilivyoelekezwa,”amesema.
“Baraza linawashauri waombaji,wazazi na walezi kuhakikisha wanaoomba vyuo ambavyo vimeorodheshwa kwenye kitabu cha mwongozo wa udahili mwaka wa masomo 2023/2024, mwongozo unaopatikana kwenye tovuti ya baraza”
Kuhusu kuanza kwa udahili, Dk Oleke amewataka wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga na kozi ngazi za Astashahada na Stashahada, kufanya maombi yao kwa umakini ili kapata nafasi ya kujiunga na programu ambazo watatimiza vigezo vyake.
“Udahili huo unaanza Mei 21, 2023 hadi Juni 30, 2023 katika awamu ya kwanza.Aidha waombaji wa programu za afya na sayansi shirikishi(Tanzania Bara),wanapaswa kuwasilisha maombi yao kupitia udahili wa pamoja (Central Admission System-CAS) katika tovuti ya baraza,”amesema Dk Oleke
“Tunawatahadharisha waombaji wa nafasi mbalimbali katika vyuo vya elimu ya ufundi wahakikishe wanafahamu vyuo vilivyosajiliwa na baraza na programu ambazo zeye ithibati na kuandika taarifa zao sahihi na kutinza taarifa watakazopatiwa na Baraza bila kumpatia mtu yoyote ili kuepusha usumbufu katika zoezi zima la maombi ya kujiunga na vyuo au programu mbalimbali,”