MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amechangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya mwaka 2023/2024,huku akitoa ombi kwa serikali kwenye mambo matatu ikiwemo kuanza ujenzi wa barabara ya Handeni-Kiblashi – Kwamtoro –Kiteto hadi Singida ili kuongeza uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
Aidha,ameiomba serikali kujenga kilomita 10 za lami kutoka Ikungi Londoni kwenda Kilimatinde Solya ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika Mgodi wa Dhahabu wa Shanta uliopo eneo la Mang’onyi.
Akichangia bajeti hiyo Mei 22,Bungeni Jijini Dodoma,Mtaturu amesema barabara hiyo ikikamilika itaongeza ufanisi katika bandari ya Tanga.
“Leo waziri ametuambia tunaenda kusaini barabara zenye urefu wa kilomita 2,035,niombe sana mkandarasi apatikane mapema kwenye barabara hii ya Handeni hadi Singida yenye urefu wa Kilomita 460 ili maboresho tuliyoyafanya kwenye bandari ya Tanga yapate majibu,
“Tumeambiwa mwezi wa sita utasainiwa mkataba nimuombe Waziri kwa heshima kabisa tuhakikishe barabara inasainiwa mapema ili wabunge wa maeneo ukitoka pale Handeni ndugu yangu Omary Kigua,ndugu yangu wa Kiteto Edward Ole Lekaita, ndugu yangu Mohammed Monni wa Chemba pamoja na mimi mwenyewe tuweze kufarijika wananchi wetu wakipata lami,”ameeleza.
Akizungumzia ombi la Kilomita 10 za lami katika Wilaya ya Ikungi amesema barabara hiyo ikijengwa itaongeza thamani ya mradi wa mgodi wa madini ya dhahabu wa Shanta.
“Mh Waziri mlinipa kilomita moja ndani ya wilaya yangu ya Ikungi,niombe sana mniongezee kilomita 10 barabara ya kutoka Ikungi Londoni kwenda Kilimatinde Solya kwa ndugu yangu Chaya ili barabara ile ijengwe kwa kiwango cha lami na kwa kuwa tuna muwekezaji pale wa madini ambaye yupo eneo la Mang’onyi,ikiwekwa lami barabara hii itaongeza thamani ya mradi ule,”amebainisha.