Baadhi ya wanufaika wa kaya masikini katika kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas
Baadhi ya wanufaika wa kaya masikini katika kijiji cha Amanimakoro wilayani Mbinga
Afisa Maendeleo ya Jamii mkoani Ruvuma Xsaveria Mlimira akizungumza na wanufaika wa kaya masikini katika kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru
JUMLA ya kaya 67,780 mkoani Ruvuma zimeendelea kunufaika na Mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Desemba 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2022 Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma zilipokea zaidi ya shilingi bilioni 7.78 zilizotolewa kwa ajili ya uhawilishaji na ufuatiliaji wa TASAF.
Amebainisha kuwa uhawilishaji wa fedha unahusisha utoaji wa ruzuku kwa kaya za walengwa hususan zenye Watoto ili ziweze kupata lishe bora na mahitaji muhimu ya shule na kupata huduma za afya.
“Mpango wa TASAF awamu ya tatu upo katika kipindi cha pili (2020-2025) cha utekelezaji ambapo katika Mkoa wa Ruvuma unatekelezwa kwenye Halmashauri zote nane,unafanyika katika vijiji na mitaa yote ’’,alisema.
Amelitaja lengo la serikali kuanzisha mpango huo kuwa ni kuziwezesha kaya masikini sana kuongeza kipato,fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii mkoani Ruvuma Xsaveria Mlimira amesema zaidi ya shilingi milioni 107 zilirudishwa TASAF makao makuu kutokana na walengwa kutofika katika malipo katika kipindi husika.
Amesema kila mwezi uhawilishaji fedha kwa kutoa ruzuku ya shilingi 12,000 kwa kila kaya masikini unafanyika ili kaya masikini ziweze kuongeza kipato kupitia uwekaji akiba na kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Mpango wa kunusuru kaya masikini hivi sasa upo katika sehemu ya pili ya utekelezaji na unahusisha vijiji na mitaa 685 katika Mkoa wa Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma