BAADHI ya wazee wa kijiji cha Nalasi na Lipepo Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma ,wameiomba Serikali kupeleka vifaa tiba na watumishi katika kituo cha afya Nalasi ili kituo hicho kianze kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Wamesema,wamechoka kutembea zaidi ya kilomita 15 kila wanapougua hadi kijiji cha Mchoteka kufuata baadhi ya huduma za matibabu na kueleza kuwa, changamoto hiyo ina wakosesha muda wa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Lipepo Ali Omari amesema, baadhi ya majengo yakiwemo jengo la wagonjwa wa nje(OPD)maabara na jengo la utawala yamekamilika,hivyo ni vyema Serikali ikafungua na kuanza kutoa huduma ili kuwapunguzia kero kwenda maeneo mengine kwa ajili ya kupata huduma.
Amesema,wamekuwa na changamoto kubwa pale mwananchi wa kijiji hicho anapozidiwa kwa homa ambayo matibabu yake yanahitaji kufika kituo cha afya kama vile upasuaji badala ya ngazi ya zahanati.
Ameongeza kuwa,katika kijiji jirani cha Nalasi kuna zahanati ndogo iliyojengwa miaka ya themanini,hata hivyo kwa sasa imeelemewa na wagonjwa kutokana na ongezeko kubwa la watu katika vijiji hivyo na baadhi ya huduma hazipatikani.
Zuberi Ali mkazi wa kijiji cha Nalasi amesema,kata ya Nalasi ni miongoni mwa maeneo ya mapito makubwa ya wanyama wakali wakiwemo Tembo ambao wamekuwa tishio kwa wananchi pindi wanapokwenda kata nyingine kufuata huduma ya matibabu.
Ali ambaye ni mjumbe wa kamati ya ujenzi wa kituo hicho amesema, katika utekelezaji wa mradi huo changamoto kubwa ni upatikanaji wa maji kwa ajili ya kazi hiyo ambapo tangu walipoanza ujenzi wake wananchi ndiyo wanaoleta maji kwa kubeba kichwani kutoka kwenye vyanzo na visima vya asili.
Hivyo ameiomba Serikali kupitia Ruwasa,kufanya mchakato wa kupata kisima kirefu cha maji ili waweze kuendelea na ujenzi wa mradi huo ambacho kitakuwa suluhisho la changamoto hiyo na kinaweza kutumika hata baada ya kituo cha afya kuanza kufanya kazi.
Kwa upande wake Muuguzi wa zahanati ya Nalasi Mwanahamisi Binamu, ameipongeza serikali kuona umuhimu wa kujenga kituo cha afya kwani kwa muda mrefu wanategemea zahanati ndogo ambayo imezidiwa na wagonjwa wanaofika kupata matibabu.
Amesema, katika zahanati hiyo baadhi ya huduma muhimu ikiwemo ya maabara hazipatikani,hivyo kushindwa kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa wanaofika kwa ajili ya kupata matibabu ambapo kwa sasa huduma zinazotolewa ni kupima malaria na virusi vya ukimwi tu.
Amesema,kwa siku wanahudumia zaidi ya watu 60 hadi 70 na akina mama wajawazito wanaofika kujifungua ni kati ya 35 hadi 40 kwa mwezi idadi ambayo kwa ngazi ya zahanati ni kubwa, na ameiomba serikali kuharakisha kuleta vifaa tiba ili kituo cha afya kianze kufanya kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando amesema,kituo cha afya Nalasi kinajengwa kutokana na fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo hadi kukamilika zaidi ya Sh,milioni 500 zitatumika.
Amesema,kwa sasa Serikali imeshaleta gari la wagonjwa na baadhi ya watoa huduma wakiwemo wauguzi na Madaktari ambao wamepelekwa katika Hospitali ya misheni Mbesa na zahanati ya Nalasi ili kupata uzoefu huku wakisubiri kufunguliwa kwa kituo hicho.
Pia amesema,wamepokea Sh.milioni 300 kwa ajili ya kununua vifaa tiba sambamba na kuagiza thamani za ofisi kutoka kwa wazabuni ambazo gharama yake ni Sh.milioni 9.
Amesema,malengo ya Halmashauri ni kukamilisha kazi zote haraka ili kituo hicho kianze kufanya kazi kabla ya mwezi Julai mwaka huu,na kuwaomba wananchi kuwa na subira kwani Serikali kupitia Halmashauri ipo kazini na itahakikisha kazi zote zinakamilika kwa muda uliopangwa.