Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefungua mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Hakimiliki nchini (COSOTA) kwa Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo pamoja na Sheria Ndogo kuhusu Kanuni za Ukusanyaji na Ugawaji wa Mirabaha ya Kazi za wasanii.
Mhe. Pindi Chana wakati akifungua mafunzo hayo Mei 18, 2023 jijini Dodoma, amesema lengo la Mafunzo hayo ni kupata uelewa wa usimamizi wa Hakimiliki na fursa za kibiashara katika masuala ya Hakimili.
“Kamati hizi zimekua chachu katika kuboresha utekekezaji wa majukumu ya Wizara, hivyo tumeona ni vyema mafunzo haya yafanyike ili tuweze kushiriki mageuzi haya katika kukuza Sekta ya ubunifu nchini” amesema Mhe. Chana.
Aidha, Mhe. Pindi Chana ameushukuru Uongozi wa Bunge kwa kutoa nafasi kwa COSOTA kutoa mafunzo kwa Wabunge hatua inayowapa fursa ya kupata uelewa wa majukumu ya Taasisi na kuwaalika Wabunge hao kujenga tasnia ya Sanaa na Taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizarani hiyo, Bw. Saidi Yakubu amesema mafunzo hayo yatakua endelevu kwa Taasisi zote za wizara ili Waheshimiwa Wabunge waelewe vyema na kusaidia katika kukuza Sekta za Wizara.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA Bi. Doreen Sinare amesema tayari Kanuni hizo zimesainiwa na zitaanza kufanya kazi tarehe moja Julai 2023.
Afisa Mtendaji Mkuu ameongeza kuwa Taasisi hiyo inajukumu la kutekeleza Ilani ya Chama tawala ya 2020-2025 ambayo inasisitiza kusimamia Hakimili na kuendesha sekta hiyo kibiashara ili wanaojihusisha na shughuli za ubunifu wanufaike na kazi zao.
Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa Taasisi hiyo tangu ihamishiwe Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo wameendelea kuimarika kwa kupata fedha za uendeshaji takriban bilioni 1.5 kutekeleza majukumu yao.