Na Mwandishi wetu, Mirerani
JENGO la soko la madini Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, la Tanzanite Trading Centre limepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi hivyo kuchochea umaliziaji wake.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linatarajia kujenga soko la madini ya Tanzanite litakalojulikana kama Tanzanite Trading Centre litakalokuwa la ghorofa tano litakalogharimu Sh5.4 bilioni.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, Baraka Kanunga amesema halmashauri hiyo imeshapokea Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo lilo.
“Tunaishukuru serikali kuu kwa kuweka kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la soko la madini, fedha ambazo zitachochea ujenzi wake kwenda kwa kasi,” amesema.
Msimamizi wa ujenzi huo, mhandisi Goodluck Masika amesema mradi huo ulianza Mei 22 mwaka 2022 na ulitarajiwa kukamilika Mei mwaka huu na jengo hilo la ghorofa tano litagharimu kiasi cha sh5.4 bilioni.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer ameishukuru Serikali ujenzi wa jengo hilo la soko la madini kwenye eneo hilo kwani litaongeza uchumi kwa jamii ya Simanjiro.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia amesema serikali inachelewesha kukamilika jengo hilo kutokana na kutotoa fedha kwa wakati.
Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Mnyawi amesema kujengwa kwa soko la madini Mirerani kutaondoa hofu ya baadhi ya watu waliodhani soko la madini litahamishwa Mirerani.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer amesema watu wa Arusha kutaka soko lirudi kwao ni sawa na kusubiri mvua inyeshe Mirerani kisha wateleze wao.