Serikali ya Tanzania imejipanga kuendelea kunufaika na fursa
zinazotokana na Mtangamano wa Kikanda ili kuwawezesha watanzania kufaidika na
uanachama wa Tanzania katika Jumuiya mbalimbali za kikanda.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Stergomena Tax wakati wa ufunguzi wa semina kuhusu “Nafasi ya Tanzania katika
Mtangamano wa Kikanda” iliyotolewa na Wizara jijini Dodoma kwa Wajumbe
wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kukuza uelewa
kuhusu masuala ya mtangamano wa kikanda.
Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa, mtangamano wa kikanda ni dhana
muhimu katika kukuza uchumi, kuimarisha uhusiano wa kisiasa, amani na usalama
katika mataifa na kwamba Kamati hiyo ni
miongoni mwa wadau muhimu wanaotakiwa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu mtangamano
wa kikanda ili kushirikiana na Wizara kueleza fursa na faida zake kwa wananchi.
Ameongeza kusema kwamba kwa Tanzania mtangamano wa kikanda ni
sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hivyo uelewa wa pamoja kuhusu
dhana hii hususan fursa, faida na changamoto na namna ya kuzitatua unahitajika
ili kufikia malengo kusudiwa.
Vilevile ameeleza kuwa, Tanzania inao mchango mkubwa katika
Mtangamano wa kikanda na inategemewa ambapo pia imeendelea kunufaika na fursa
mbalimbali zinazotokana na uanachama wake katika Jumuiya za Kikanda hususan,
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
ikiwemo ajira, biashara, teknolojia, elimu na uwekezaji.
Mhe. Dkt. Tax pia alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kila
Jumuiya kwa kusisitiza kuwa kila Jumuiya ina umuhimu na mchango mkubwa kwa
Tanzania kulingana na lengo la kuanzishwa kwake.
“Naomba niweke hoja hii sawa. Kumekuwa na ulinganifu wa
utendaji wa Jumuiya hizi ambapo baadhi ya watu wanaona jumuiya moja ni bora
kuliko nyingine pasipo kujua kwamba kila moja ina umuhimu wake kulingana na
lengo la kuanzishwa,” amesema Dkt. Tax.
Akitoa mfano amesema SADC ilianzishwa kwa lengo la kupigania
ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Hivyo kwa kiasi kikubwa Jumuiya hii imejikita kwenye masuala ya amani, ulinzi
na usalama na kwamba ni kutokana na lengo hilo nchi za kusini zilikombolewa
katika ukoloni lakini pia nchi wanachama kama Madagascar na Lesotho zilizokuwa
na migogoro zimerejea katika hali ya amani na utulivu.
Kuhusu EAC amesema lengo la kuanzishwa kwake lilikuwa ni
kuimarisha uchumi na biashara, hivyo kila jumuiya ni muhimu kulingana na
majukumu yake.
Pia amesema anaishukuru kamati hiyo kwa kuendelea
kushirikiana na Wizara kwenye masuala mbalimbali yenye maslahi kwa nchi na
kuahidi kuendelea kushirikiana nayo katika masuala mbalimbali yanayohusu
utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.
Akiwasilisha mada hiyo, Mkufunzi kutoka Chuo cha
Diplomasia cha jijini Dar es Salaam, Bw. Charles Mtakwa amesema zipo faida
nyingi kwa Tanzania kuwa mwanachama katika EAC na SADC ikiwemo ajira, biashara,
elimu, teknolojia na uendelezaji miundombinu ya kikanda.
“Mtangamano wa Kikanda ni dhana muhimu kwa Tanzania na hususan
katika kukuza uchumi kupitia biashara, uwekezaji lakini pia kuboresha ufanisi
wa soko la bidhaa mbalimbali kwani ni muhimu kwa nchi za Afrika kuendelea
kukuza biashara miongoni mwake ambayo bado ipo katika kiwango cha chini cha
asilimia 13 ukilinganisha na nchi za Bara la Asia asilimia 61 na Amerika
asilimia 47” amesema Bw. Mtakwa.
Amesema kupitia Mtangangamano wa kikanda nchi wanachama
huweza kufanya maamuzi ya pamoja ya kisera na kuchochea mageuzi ikiwemo yale ya kiuchumi. Pia kupitia
mtangamano wa kikanda nchi wanachama hushirikiana kuchangia gharama za miradi
mikubwa na miundombinu kama miradi ya umeme na miradi ya barabara na reli.
Ameeleza kuwa, Mtangamano wa Kikanda ambao unalenga katika
kuziwezesha nchi wanachama kushirikiana katika masuala mbalimbali unazo hatua tano ambazo ni biashara huria;
muungano wa forodha;soko la pamoja;muungano wa kifedha na muungano wa kisiasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya
Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa amesema kuwa anaipongeza na kuishukuru
Wizara kwa kuendelea kutoa semina kuhusu mada mbalimbali za umuhimu na kwamba
Kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano na ushauri unaohitajika kwa Wizara.
Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati hiyo wameishauri Wizara
kushirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kutangaza fursa zinazopatikana
katika mtangamano wa kikanda na kuendelea kusimamia makubaliano na mikataba
iliyokwisha sainiwa katika kanda hizo ili itekelezwe kama ilivyopangwa.
Semina ikiendelea |
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakifuatilia semina kuhusu Mtangamano wa Kikanda |
Semina ikiendelea |
Washiriki wakifuatilia semina |
Mkutano ukiendelea |