Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene,akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 16,2023 jijini Dodoma kuelekea mkutano wa Makatibu Muhtasi na Watunza kumbukumbu utafanyika Visiwani Zanzibar kuanzia Mei 22 hadi 27 mwaka huu.
Na.Alex Sonna-DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Dk Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Makatibu Muhtasi na Watunza kumbukumbu utakaofanyika Visiwani Zanzibar.
Hayo yamesemwa leo Mei 16,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema kuwa kwa mara ya kwanza mkutano huo utafanyika Visiwani Zanzibar kuanzia Mei 22 hadi 27 mwaka huu.
Simbachawene amesema kuwa Lengo la Mkutano huo ni kujadili majukumu mbalimbali ya kitaaluma ya wanachama wa vyama hivyo viwili ili kuleta ufanisi wa kada hiyo katika Sekta ya Umma.
”Mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya elfu nane (8000) na utafanyika Visiwani Zanzibar kuanzia Mei 22 mpaka 27 ,2023 na Mgeni Rasmi katika Ufunguzi atakuwa Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.”amesema Waziri Simbachawene
Aidha Waziri Simbachawene,amewataka Waajiri wote wa Taasisi za Umma kuwaruhusu na kuwagharamia Wanachama wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya kumbukumbu na Nyaraka Tanzani (TRUMPA) na Wanachama wa Chama Cha Makatibu Muhsusi (TAPSEA) kushiriki Mkutano wao.
“Kama mtakumbuka Novemba 27,2022 ,Mheshimiwa Rais wakati akifungua Mkutano wa Kumi wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA)uliofanyika Jijini Arusha alitoa maagizo kuwa ufanyike Mkutano Mkubwa kwa kuwaunganisha wanachama wa vyama vyote viwili yaani TRAMPA na TAPSEA tena akasema ufanyike Zanzibar na akaelekeza waajiri wawaachie wanachama hao kushiriki kwa wingi ili kujadili majukumu yao na umuhimu wa kada hiyo katika ustawi wa Utumishi wa Umma,”amesema Simbachawene
Hata hivyo Mhe.Simbachawene amesema kuwa katika Mkutano huo Wanachama wote watakaohudhuria Watakula kiapo kwa ajili ya kutumikia nafasi zao lengo likiwa ni kuwaonesha na kuwakumbusha umuhimu wa kada hizo katika Utumishi wa Umma.
“Wote watakula kiapo ili waweze kutunza siri za Serikali katika taasisi zao na kusitokee kuvija kwa siri yeyote kwa namna yeyote ile ndio maana nazidi kuwakumbusha Waajiri kuhakikisha watumishi wao wanashiriki mkutano huo kwani ni muhimu kwa ustawi wa Taifa,”amesema Mhe.Simbachawene
Mhe.Simbachawene amesema kila taasisi ina Mfumo wake wa Utunzaji kumbukumbu iwe ni umma au Binafsi ila lengo ni kulinda Maslahi ya taasisi yenyewe ndio maana Watunza Kumbukumbu na Makatibu Mahsusi ni viungo muhimu sana katika Ustawi wa Taasisi.