Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer, ameitaka jamii ya eneo hilo kulinda ardhi waliyonayo kama mboni ya jicho kwani huo ndiyo urithi wao.
Kiria akizungumza kwenye maadhimisho ya wiki ya wazazi amesema ardhi ndiyo ambayo imetoa ajira kubwa kwa watanzanina kupitia kilimo na ufugaji hivyo itunzwe.
Amesema ni makosa makubwa kuuza ardhi kiholela hivyo jamii ya wana Simanjiro wanapaswa kutambua hilo na kutojihusisha na uuzaji wa ardhi bila sababu maalum.
Ameeleza kuwa wana Simanjiro wanapaswa kuyaishi maneno ya waasisi wa Taifa juu ya kulinda ardhi kama mboni ya jicho kwani ndiyo imetoa ajira kwa watanzania wengi.
“Wazee wetu hayati mwalimu Julius Nyerere na sheikhe Abeid Amani Karume, nyakati za uhai wao walisimama kidete kupinga uuzaji holela wa ardhi hivyo tunapaswa kusimamia hilo,” amesema Kiria.
Amesema kero ya uuzwaji wa ardhi Simanjiro amekuwa akiizungumzia na kuipigia kelele kila wakati kwani ndiyo mustakabali wa uchumi wa jamii hasa ya hali ya chini.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima ameunga mkono kauli hiyo ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro hivyo anamuunga mkono juu ya utunzaji ardhi.
“Ardhi ndiyo urithi wetu wafugaji na wakulima hivyo tuhakikishe tunayafuatilia na kuyatilia maanani haya tunayoyasema ili miaka ijayo tusije tukajutia,” amesema Toima.