Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Mkoani Manyara, Peter Toima amewataka wanachama wa chama hicho watambue kuwa CCM ni taasisi ya watu wote ambao ni wanachama wa chama hicho na siyo mali ya mtu mmoja.
Toima ameyasema hayo mara baada ya baadhi ya wanachama wa CCM tawi la Kitiangare, kijiji cha Sukuro, kata ya Komolo wilayani Simanjiro, kubeba mabango ya kupinga uchaguzi wa tawi hilo.
Baadhi ya wanachama wa tawi hilo walibeba mabango hayo na kusimamisha msafara wa Naibu katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi Taifa (Zanzibar) Othman Ally Maulid, ulipopita eneo hilo kwenye maadhimisho ya wiki ya wazazi.
Toima amesema wanachama hao watambue kuwa, CCM siyo mali ya mtu mmoja anayetaka kupanga safu na kambi yake kwa ajili ya uchaguzi ujao, hivyo waridhike na matokeo hayo.
“Ukiwa mwanachama wa CCM, mjumbe akishachaguliwa kwa nafasi yeyote tunapaswa kukubali baada ya matokeo kutoka na tuache ubishi wa miaka mitano hautasaidia,” amesema.
Amesema wanachama hao watambue kuwa uchaguzi wa tawi hilo umeshafanyika na wanapaswa kuendelea na utaratibu mwingine wa maendeleo na siyo migogoro ya uchaguzi.
“Tunapaswa kubadilika wana Kitiangare kwani mwanachama mwenzetu akishinda kuna shida gani, au hawa walioshinda kwani wametoka nje ya tawi lenu?” amehoji Toima.
Diwani wa kata ya Terrat, Jackson Ole Materi amesema ukiangalia mabango yote utaona hati imefanana ni mtu mmoja ameandika mabango hayo na watu kupewa ili wabebe.
“Hata mbebaji bango ukimuuliza alichobeba kimeandikwa maneno gani anashindwa kujibu kwa sababu hajui chochote kilichoandikwa zaidi ya kuambiwa abebe tuu,” amesema Materi.
Diwani wa kata ya Ngorika, Albert Msole amesema matawi kama hayo yanayosumbua na kusababisha kelele zisizo na maana dawa yake ni kufutwa tuu ili kuyakomesha.
Katibu wa CCM wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba amesema uchaguzi umeshafanyika na viongozi halali wameshapatikana, hivyo wanachama hao wanapaswa kuangalia maendeleo mengine.