Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa kushika nafasi ya 26 kidunia na ya pili barani Afrika baada ya Mauritius.
Hayo yamebainishwa kwenye utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu ukomavu wa matumizi ya Teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index)
Ripoti hiyo ambayo inatokana na utafiti uliofanyika mwaka 2022 katika nchi 198 duniani, inabainisha kuwa Tanzania imefanikiwa kupanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A na kushika nafasi ya 26 ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo ilishika nafasi ya 90.
Kwa upande wa Afrika, utafiti huo ulihusisha nchi 49 ikiwemo Tanzania na matokeo yamebaini kuwa, matumizi ya TEHAMA nchini yamepanda na kufikia asilimia 0.86 wakati Mauritius ina asilimia 0.864.Tanzania imepanda kutoka nafasi ya tano mwaka 2021 ambapo ilikuwa nyuma ya Afrika Kusini, Ghana, Kenya and Rwanda hadi nafasi ya pili mwaka 2022.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania imekuwa kinara kati ya nchi 13 zilizofanyiwa utafiti ambazo ni Burundi, Comoros, Djibouti, Somalia, Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan, Eritrea, Kenya, Uganda, Rwanda, Seychelles na Tanzania ambapo matokeo yanaonyesha kuwa Tanzania imepanda kutoka nafasi ya tatu mwaka 2021 hadi nafasi ya kwanza mwaka 2022.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa mwezi Machi mwaka huu, sekta za elimu, afya, fedha na kilimo nchini Tanzania ni sekta zinazoongoza katika utoaji wa huduma za serikali kupitia TEHAMA na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi.
Aidha, ripoti hiyo imebainisha kuwa, mafanikio hayo yanatokana na utayari wa serikali wa kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma, uwepo wa dira mahususi kuhusu sera ya TEHAMA, Sheria, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao, mikakati madhubuti na utekelezaji wake unaosimamiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).
Utafiti huo uliangalia maeneo manne ambayo ni mipango na usimamizi wa TEHAMA serikalini ikiwa ni pamoja na uwepo wa Miundombinu ya Kuhitafadhia Mifumo (Data Centers), Miongozo ya kubadilishana taarifa kwa mifumo ya Serikali na uwepo wa mifumo shirikishi, ushirikishwaji wa wananchi kupitia majukwaa ya kidijitali kwa kupima utaratibu unaotumika kwa wananchi kutoa maoni kwa njia ya kidijitali, majukwaa ya kidijitali yanayotumika kushirikisha wananchi, taarifa za wazi pamoja na tovuti za Serikali.
Eneo la mwisho lililoangaliwa ni uwepo wa nyenzo wezeshi za teknolojia serikalini kwa kuangalia Sera ya ubunifu wa teknlojia, sheria na kanuni, ujuzi katika masuala ya dijitali na programu mbalimbali zinazotumika kuimarisha TEHAMA serikalini.
Aidha, utafiti huo umetaja mifumo ambayo imesaidia kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma nchini kuwa ni pamoja na mfumo wa e-Mrejesho ambao unawawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Taasisi za umma kwa njia ya kidijitali, ili kuwasilisha maoni, mapendekezo, maswali, pongezi au malalamiko yao sambamba na kufuatilia utekelezaji wake ndani ya Taasisi husika.
Mifumo shirikishi katika Taasisi za Umma Vituo vya kuhifadhia Mifumo (Government Data Centers) Mifumo hiyo ni pamoja na Mtandao wa Mawasiliano Serikalini ambao umeziunganisha Wizara, Idara na Wakala 72 pamoja na Halmashauri 77, Kituo cha kuhifadhia data cha serikali, Mfumo wa e-Office ambao huwezesha na kurahisisha shughuli za utawala za kila siku ndani ya Taasisi za umma ikiwa ni pamoja na mzunguko wa nyaraka ndani ya Taasisi.
Mifumo mingine ni huduma za mtandao ambazo hurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi kidijitali, huduma hizo ni pamoja na Ajira portal, Mfumo wa Malipo Serikalini (GePG), Maombi na utoaji wa leseni, hati ya kusafiria n.k.
Vilevile, Mfumo wa MGOV ambao ni mfumo jumuishi wa utoaji wa huduma kwa njia ya simu za mkononi Serikalini, mfumo huu unarahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma. Mfumo wa mGOV umeunganishwa na watoa huduma wote wa simu za mikononi nchini Tanzania na unatoa huduma za ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kupitia namba jumuishi 15200 na 15201 pamoja na huduma za menyu ya USSD kupitia namba jumuishi *152*00#.
Aidha, mfumo wa MGOV unaruhusu Taasisi za Umma kutoa huduma kupitia namba binafsi za Taasisi, mfano wa namba binafsi za Taasisi ni 199 ya Wizara ya Afya inayotoa huduma na taarifa za COVID-19, na *113# ya PCCB inayotoa huduma ya kuripoti matukio ya rushwa. Hadi kufikia Julai, 2022 Taasisi zaidi ya 254 zinatumia mfumo wa mGOV kutoa huduma, baadhi ya huduma hizo ni SMS za manunuzi ya umeme (LUKU), SMS za huduma za malipo ya Serikali (GePG), Huduma za kikodi (TRA), Huduma za Ardhi, Huduma za afya (NHIF, CHF) nk.
Pia, Mfumo wa GoVESB ambao ni Mfumo shirikishi unaounganisha mifumo ya Taasisi za Umma kuwasiliana na kubadilishana taarifa, Mfumo huu unatumika kupunguza urudufu wa mifumo pamoja na kurahisishsa utendaji kazi wa taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mingine ni Mfumo wa ukusanyaji wa malipo Serikalini (GePG), Mfumo wa ‘Ajira Portal’ ambao hurahisisha utoaji wa matangazo na maombi ya nafasi za kazi kwa njia ya kidijitali. Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE), Mfumo wa taarifa za Usimamizi wa Ushuru na forodha (TANCIS), Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Watumishi Serikalini (HCMIS), Mfumo wa manunuzi mtandaoni (TANePS) na Tovuti Kuu ya Serikali.
Licha ya kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA nchini, ripoti hiyo imebainisha kuwa pengo la kidijitali limeongezeka katika nchi masikini zenye uchumi wa chini na wa kati kutokana na uhaba wa fedha pamoja na kutokuwepo kwa sera madhubuti kuhusu TEHAMA. Utafiti huu umekuwa na manufaa kwa mataifa mbalimbali kwakuwa unaangalia zana zinazotumika katika kuimarisha TEHAMA kwenye mataifa mbalimbali pamoja na kuainisha maeneo yanayotakiwa kuboreshwa zaidi.