Waogeleaji a klabu ya FK Blue Marlins katika picha ya pamoja
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Jumla ya klabu 13 zitashiriki katika mashindano ya kwanza ya kuogelea ya FK Blue Marlins yaliyopangwa kuanza Jumamosi (Mei 13) kwenye bwawa la kuogelea la shule ya kimataifa ya FK ya Bahari Beach.
Klabu hizo ni Dar Swim Club, Bluefins, Taliss-IST, Lake Swim Club na Champion Rise Club. Klabu nyingine ni Wahoo Zanzibar, Braeburn Sharks, Pigec Swim Club, Majimaji, Mis Piranhas, Premier Swim Club , Train To Gain, na wenyeji FK Blue Marlins.
Meneja wa klabu ya FK Blue Marlins Opalina Nanyaro alisema kuwa jumla ya waogeleaji 232 watashindana katika mashindano hayo ambayo yatamalizika Jumapili ya Mei 14.
Opalina alisema kuwa zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na RDB Bank Foundation, FK International Schools, GardaWorld, EFM Company Limited, K-15 Photos, Coca Cola Kwanza Limited, Just Fit na the Duke Media.
Alisema medali zitatolewa kwa waogeleaji watatu bora. Zawadi hizo ni dhahabu, fedha na shaba. Vikombe vitatunukiwa washindi wa makundi mbalimbali. Medali pia zitatolewa kwa timu zitakazoshinda katika mashindano ya relei.
Kwa mujibu wa Opalina waogeleaji watashindana katika umri tofauti katika staili mbalimbali pamoja na relei. Staili hizo ni Individual Medley (IM), butterfly, backstroke, breaststroke, na freestyle.
Waogeleaji wa kike watashindana katika makundi ya umri tofauti ambapo kundi la kwanza ni kwa watoto wenye miaka nane kushuka chini, miaka tisa na kumi, 11 na 12, 13 na 14 na zaidi ya miaka 15 wakati makundi ya waogeleaji wa kiume ni miaka nane kushika chini, miaka, 9 na 10, 11 na 12, 13 na 14, na zaidi ya miaka 15.