Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima (kushoto) akivishwa zawadi ya vazi la jadi na Diwani wa Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro, Ezekiel Lesenga Mardadi, kwenye maadhimisho ya wiki ya jumuiya ya Wazazi kitaifa na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA la ECTAT Foundation lililopo Kata ya Emboreet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, limetumia shilingi bilioni 25 kujenga shule 38 za msingi kwenye mikoa mitano na wilaya tisa nchini.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara, Peter Toima ambaye pia ni Mwenyekiti wa ECLAT Foundation, ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya wiki ya jumuiya ya wazazi wa CCM kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro.
Toima amesema shirika hilo limejenga shule hizo za msingi nchini kwa lengo la kusaidia jamii kupata uelewa kwenye wilaya na mikoa mbalimbali nchini zenye changamoto ya shule.
Ametaja wilaya ambazo wamejenga shule hizo 38 za msingi ni Simanjiro, Kiteto, Mbulu na Hanang’ mkoani Manyara, Monduli na Ngorongoro mkoani Arusha, Tandahimba mkoani Mtwara, Muleba mkoani Kagera na Ruhangwa mkoani Lindi.
“Tumetumia kiasi cha Shilingi bilioni 25 kujenga shule hizo 38 nchini, hapo hatujahesabu ujenzi wa shule za sekondari na chuo cha ufundi stadi (veta),” amesema Toima.
Amesema shirika la ECLAT Foundation linahudumia jamii nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na kuwezesha vikundi vya wanawake kwa lengo la kuwajengea uwezo.
Hata hivyo, Naibu Katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi Zanzibar, Othman Ally Maulid, amesema kitendo cha Toima kujenga shule hizo ni sawa na kutoa sadaka kwani ni jambo endelevu.
“Umeisaidia serikali ili watoto wapate elimu hivyo umetoa sadaka kwenye eneo lako na kwa watanzania kwa ujumla, bila kujali kabila, dini, au eneo hivyo kila mtu atakuombea,” amesema Maulid.
Hata hivyo, ametoa ombi kwa Toima kugeukia pia upande wa Zanzibar kwa kuwasaidia kuwajengea shule kama shirika lake lilivyofanya kwenye maeneo mbalimbali upande wa bara.
Diwani wa kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga Mardadi amesema jamii ya eneo hilo imefanikiwa kujengewa shule za msingi na shirika la ECLAT Foundation hivyo wanalishukuru.
“Tunamshukuru mno, pamoja na kuwa ni msomi aliyetoka jamii ya kifugaji hakusahau kujenga shule kwao ndiyo sababu tumemchagua kuwa Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wetu,” amesema Mardadi.