MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ametoa mifuko ya saruji 400 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 8 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa hosteli ya sekondari ya Dkt Ally Mohammed Shein iliyopo kata ya Misughaa wilani Ikungi Mkoani Singida.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake aliyowahi kuitoa ya kuanza ujenzi wa hosteli haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuwapunguzia adha wanafunzi wa shule hiyo hasa wa kike kutembea umbali mrefu kufika shuleni.
Mbali ya kukabidhi saruji hiyo pia ametoa kompyuta nne pamoja na projekta moja ili iweze kuwasaidia wanafunzi wa shule hiyo ambayo ni miongoni mwa zinazofanya vizuri kimasomo wilayani humo.
Akikabidhi vitu hivyo Mei 8,2023,shuleni hapo Mtaturu amesema anatoa msaada huo ikiwa ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombninu ya shule na kuwawezesha kusoma bila ada kwa shule za msingi na sekondari.
“Leo hii nimeleta saruji mifuko 100 kwa ajili ya uzinduzi wa ujenzi na mifuko yote 400 nimekwisha ilipia ,lengo langu nataka tuanze haraka kufanya mchakato wa kuanza ujenzi ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),yam waka 2020/2025,”
Rais wetu amefanya kazi kubwa ya kutoa fedha nyingi katika nchi yetu kwa ajili ya kutekeleza miradi mingi ya maendeleo,na jimbo letu la Singida Mashariki likiwa ni mnufaika ya fedha hizo,hivyo sisi tukiwa ni wawakilishi wa wananchi tunakila sababu ya kumuunga mkono na kumsaidia,”.ameongeza.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Jackson Maruma amemshukuru mbunge Mtaturu kwa msaada alioutoa na kueleza kuwa sio mara yake ya kwanza kufanya hivyo.
“Mh.Mtaturu ameweza kufanikisha kupatikana kwa mnara wa simu wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL),ambapo sasa tunapata huduma za intaneti katika kata nzima na sisi ni wanufaika kwa kufundisha wanafunzi masomo mbalimbali,”amesema.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Athuman Kitiku akitoa neno la shukrani ameema maboresho yaliyofanyika shuleni hapo hayawezi kumfanya mzazi anayesomesha mtoto wake katika shule hiyo kujuta,na yote yanatokea kutokana na mchango mkubwa alioutoa mbunge huyu Mtaturu,ameeleza.
Februari 29,2020,Mtaturu alikabidhi kompyuta tano,printer moja na panel ya umeme jua tatu vyenye thamani ya Shilingi Milioni 11.2 kwa shule.