Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Mwaka 2021 sekta ya kilimo inatajwa kukua kwa asilimia 3.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.9 katika mwaka 2020. Vilevile, sekta hiyo imechangia asilimia 26.1 katika Pato la Taifa, imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda. 26.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa mwaka 2023/2024.
Aidha kwa upande wa mazao, Waziri Bashe alisema “Sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 3.6 mwaka 2021 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5 mwaka 2020 ambapo imechangia asilimia 14.6 kwenye Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 15.4 mwaka 2020 na imeendelea kuchangia asilimia 100 ya upatikanaji wa chakula. Aidha, mazao ya kilimo yamechangia takribani dola za Marekani bilioni 1.38 ya mauzo nje ya nchi”.
Hata hivyo kufuatia mwenendo wa ukuaji wa idadi ya watu ndani ya nchi na duniani ifikapo mwaka 2050, Waziri Bashe alisema kuwa Tanzania itakuwa na idadi ya watu milioni 136 na dunia itakuwa na watu bilioni 9.7. Katika kipindi hicho, uzalishaji wa chakula duniani unakadiriwa kupungua kwa asilimia 4 wakati mahitaji halisi ya chakula yanakadiriwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 50.
“Ili kuwa salama kwenye eneo hili ni lazima kuendelea kuwekeza katika mifumo imara na himilivu ya kilimo inayotumia teknolojia za umwagiliaji za kisasa, uwezo wa kuhifadhi mbegu zetu za asili ili kuwa msingi imara wa kufanya utafiti kupata teknolojia bora za uzalishaji wa mbegu ili kujihakikishia usalama wa chakula na ulinzi wa uchumi wetu”. Alisisitiza Waziri Bashe.