Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Lameck Michael Mlacha ameongoza kikao cha Menejimenti katika Kanda hiyo kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa robo mwaka ya Januari hadi Machi,2023 lengo likiwa ni kuboresha zaidi huduma ya utoaji haki katika Kanda hiyo.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Jaji Mlacha aliwataka wajumbe pamoja na watumishi wote wa Mahakama katika Kanda hiyo kujitathmini na kuchukua hatua za mabadiliko chanya ya kuboresha utendaji kazi.
“Siku chache zilizopita niliwaletea maelekezo ya Mhe.Jaji Kiongozi ambayo kwa ufupi yanahusu kuboresha mikakati ya kumaliza mashauri ya mlundikano. Maelekeo hayo yanatakiwa yatekelezwe na kutolewa taarifa kama tulivyoagizana” alisema Mhe Mlacha.
Jaji Mfawidhi huyo aliwakumbusha viongozi na watendaji kushiriki kikamilifu katika kutekeleza yale yote yanayoazimiwa na kikao ikiwa ni pamoja na maelekezo mbalimbali ya Viongozi Wakuu wa Mahakama ya Tanzania ambayo yanatolewa siku hadi siku.
Tathmini hiyo ya utendaji kazi ilionesha kuwa Kanda ya Kigoma inaendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa jukumu kuu la utoaji haki ambapo matumizi ya TEHAMA yameendelea kuimarika katika kusajili mashauri na kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao.
Taarifa ya utendaji kazi ya robo mwaka ilibainisha kuwa kati ya Januari hadi Machi, 2023, Kanda ilivuka mwezi Desemba, 2022 na mashauri 774, ikapokea mashauri 2,319 na kumaliza mashauri 1,997. Ambapo kasi ya umalizaji wa mashauri “Clearance rate-CR” ikiwa ni 86.
Hata hivyo, wajumbe wa kikao hicho walikubaliana kuwa kiwango cha umalizaji wa mashauri bado kipo chini na kwa upende mwingine, taarifa ilionesha kuwa katika kipindi hicho jumla ya mashauri 353 yalisikilizwa kwa njia ya mtandao na kujiwekea Mkakati wa kuvuka mashauri 826 yaliyosikilizwa kwa njia ya mtandao mwaka 2022.
Aidha, katika kikao hicho, Mhe. Mlacha alitangaza mabadiliko ya nafasi ya Mtendaji wa Mahakama ambapo alitambulisha Bw.Benjamin Mlimbila kuwa Mtendaji mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigomna aliyehamia kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara. Bw. Mlimbila anakuchukua nafasi ya Bw. Moses Mashaka aliyehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa Mtendaji wa Kanda hiyo.
Kikao kilijikita katika kujipima juu ya utendaji kazi ikilinganishwa na viwango vya utendaji kazi vilivyowekwa na Mahakama ya Tanzania na pia Mpango Mkakati wa awamu ya pili (2020/2021 hadi 2024/2025).
Washiriki wa kikao hicho ni pamoja na wajumbe kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma na Mahakama za Wilaya sita pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akifafanua jambo wakati wa kikao cha Menejimenti kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mahakama kuu hiyo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (kulia) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga wakiwa katika picha ya pamoja wakifuatilia kwa makini taarifa ya utekelezaji wa majukumu iliyotolewa katika kikao hicho.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Venance Katoke Mwakitalu (wa kwanza kulia), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao hicho wakisikiliza kwa makini maelekezo kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo (hayupo katika picha).
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kibondo, Mhe. Maila Makonya (aliyesimama) akifafanua jambo kuhusu utekelezaji wa maazimio ya utendaji kazi wa Wilaya yake kwenye Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (katikati) akiwa katika picha ya pamoja ni Kamati ya uongozi Mahakama Kanda ya Kigoma ikiongozwa na , Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga, wa pili kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw.Benjamin Mlimbila, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Maliki na wa kwanza kulia aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama hiyo aliyehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka.