Na Mwandishi Wetu -WNN
MKURUGENZI wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bi. Miriam Mmbaga,amewataka Maafisa Utumishi na Utawala na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kuhakikisha kuwa Watumishi wanawezeshwa kutekeleza majukumu yao vizuri badala ya kuwasubiri wakosee ili kuwafungulia mashtaka.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya Maafisa Utumishi na Utawala kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo.
“Idara za Utumishi na Utawala ndio zinazowezesha Watumishi wengi waweze kufanya kazi vizuri na kuiwezesha Wizara kutimiza malengo yake. Sisi tuliopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunawahudumia watumishi walio Raia na ambao ni Askari. Hatuna budi kuhakikisha kuwa tunapata mafunzo ya mara kwa mara ili kupata ujuzi zaidi katika kushughulikia masuala ya kinidhamu ya Watumishi na kutenda haki kwa mujibu wa kanuni na sheria zinazotuongoza katika kusimamia masuala ya kinidhamu.”alisema Miriam.
Bi Miriam amesema kuwa katika kushughulikia mchakato wa mashauri ya Kinidhamu ni vyema Mamlaka za Kinidhamu dhidi ya Watumishi kuzingatia Sheria za Utumishi wa Umma na pia kabla ya kuanzisha mchakato wa nidhamu uchunguzi wa awali ufanyike ili kuweza kujiridhisha na kufanya maamuzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti baadhi ya Maafisa Utumishi akiwemo Ernajoyce Hallo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Ally Shemahimbo kutoka Jeshi la Polisi wamesema kuwa mafunzo haya ni muhimu kwani yatawajengea uwezo wa namna bora ya kushughulikia masuala ya kinidhamu ya Watumishi ambayo yakemukua yakijitokeza ndani ya Tume na katika Wizara.
Pia wamesema mafunzo yatawasaida kuwajengea uwezo kuwashauri Viongozi wao namna bora ya kuwasaidia Watumishi na kuwachukulia hatua sahihi Watumishi pindi wanapokuwa wamekosea bila kumwonea Mtumishi na kutoathiri taswira ya Taasisi.
Hilda Tegwa ni Mkurugenzi Msaidizi Rasilimaliwatu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye yeye ameshauri baadhi ya Sheria katika kusimamia masuala ya kinidhamu ya Watumishi hususani kupitia Viongozi kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha usalama wao katika kusimamia masuala ya Kinidhamu.