Na Mwandishi wetu, Mirerani
WANACHAMA wa Nyanza Group wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, wametoa vifaa vya afya, usafi kwenye kituo cha afya Mirerani na kuchangia vyakula kituo cha watoto yatima cha Light In Africa.
Mwenyekiti wa Nyanza Group iliyoanzishwa mwaka 2012 mji mdogo wa Mirerani, Malimi Kija amesema mioyo ya hisani na kujitolea imewasukuma kusaidia kituo cha afya na watoto hao.
Amesema kikundi chao chenye wanachama 100 kinaiunga mkono serikali kwa kujitoa kupitia mifuko yao kwenye changamoto za kijamii ili wahitaji hao wajisikie kama binadamu wa kawaida.
“Tunatoa kidogo tulichopata na kuwapa wahitaji nao wapate faraja kama watanzania wenzetu wanapopata changamoto tunahusika nao ili kuwafariji na kujisikia faraja pindi tukiwasaidia,” amesema Kija.
Amesema kikundi chao kinapenda jamii inayowazunguka na wanafanikisha hayo kupitia kauli mbiu yao Nyanza Group ya tunawezeshana na kufikia jamii katika mahitaji.
Katibu wa Nyanza Group, mwalimu Daniel Ndaikya amesema misaada hiyo ambayo imetolewa kwenye kituo cha afya Mirerani na kituo cha watoto yatima cha Light In Africa imegharimu kiasi cha shilingi milioni 1.5.
Ndaikya amesema fedha hizo zimetokana na michango yao binafsi kwa kuchangia mmoja mmoja kupitia Nyanza Group ili kusaidia jamii inayowazunguka kwenye mji huo mdogo wa Mirerani.
Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya amewapongeza wanachama na viongozi wa Nyanza Group kwa kujitolea misaada hiyo.
“Jamii inapaswa kuiga mambo mazuri kama haya ya Nyanza Group kusaidia wahitaji bila kusubiri serikali ifanye kila jambo kwani lengo ni kuhakikisha wahitaji wanatimiziwa na kupata watakacho,” amesema Mgaya.