Na Gideon Gregory-DODOMA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah, amesema vifaa vyote vinavyohitajika kukamilisha miradi ya Serikali ikiwemo mfumo wa umeme, maji, uzimaji wa moto tayari vimekwishawasili katika miradi yote wanayosimamia.
Bw.Abdallah ameyasema hayo wakati akikagua miradi ya ujenzi wa Majengo ya Ofisi za Serikali eneo la Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Amesema wataendelea kuongeza timu ya wafanyakazi ili kufidia muda uliokuwa unapotea, badala ya kufanya kazi kwa masaa 12 wataenda kufanya kwa muda wa masaa 24 ili miradi iweze kukamilika kwa muda uliopangwa.
“Matarajio yetu ni kukamilisha kazi kwa muda ulikusudiwa, tutaenda kujadiliana ili tuweze kuona ni muda gani utakuwa ni wa nyongeza kidogo na kwa kiwango sahihi, ndiyo maana leo mnaniona saiti sitaki kukaa ofisini niwe naletewa taarifa ndiyo maana nakuja mwenyewe kukagua,”amesema Bw.Abdallah.
Hata hivyo ameagiza miradi hiyo ikamilike kwa wakati ikiwemo mradi wa nyumba za makazi 100 Chamwino ambao umekamilika ukiwa katika hatua za mwishon na mwishoni mwa mwezi huu zitakuwa zimekamilika.
Ameongeza kuwa wako kwenye majadiliano na Wizara husika zilizotoa zabuni za kufanya kazi hiyo ili kuangalia namna ya kuharakisha kasi ya utendaji kazi katika miradi hiyo.
“Na mchana wa leo nitakuwa na mkutano na timu yote inayosimamia miradi kuweza kupitia hatua kwa hatua, ni changamoto gani ambazo tumekutana nazo eneo la ujenzi na ni namna gani tunaweza kukabiliana nazo,”ameongeza.
Kabla ya kukagua miradi ya Mji wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu pia alipata fursa ya kufanya ziara kwenye Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Wakala wa Manunuzi Serikalini GPSA ambacho pia kipo katika hatua za mwisho na akaonyesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi.