Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Ole Materi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyofanikisha maendeleo kwenye eneo hilo.
Materi amesema hivi sasa kuna miradi mingi ya maendeleo kwenye kata ya Terrat hivyo wananchi wanamshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa namna alivyowatendea.
Amesema kata hiyo imepatiwa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 unaonufaisha wananchi wa vijiji vya Terrat na Engonong’oi.
“Pamoja na kunufaisha binadamu mradi huo wa maji pia utawanufaisha mifugo kwani kuna mabirika mawili ya kunyweshea ng’ombe,” amesema Materi.
Amesema kwenye sekta ya elimu wamejengewa madarasa mawili ya shule ya sekondari Terrat kupitia fedha za (PFR) na UVIKO-19.
“Pia madarasa mawili shule ya msingi Terrat yamefikia hatua ya boma na Serikali imetoa shilingi milioni 25 ya kumalizia na imeshapauliwa,” amesema Materi.
Amewapongeza wananchi kwa kujenga matundu sita ya vyoo kwenye shule ya msingi Engonong’oi na kufikia hatua ya lenta hivyo wanaisubiri Serikali kuikamilisha.
Amesema pia wananchi kwa nguvu zao wamejenga zahanati kwenye kijiji cha Losakwi na kufikia hatua ya boma na Serikali imewapatia shilingi milioni 50 ya kumalizia.
“Pia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia imetujengea kituo cha afya kata ya Terrat kitakachosaidia wananchi kupata huduma ya afya,” amesema Materi.
Hata hivyo, amesema watasimama kidete kumuunga mkono Rais Samia na watapambana na wanaobeza na kupinga maendeleo yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita.
“Tunamuunga mkono Rais Samia kwani tunatambua mama anaupiga mwingi kutokana na maendeleo mbalimbali yanayoonekana iwe katika sekta ya maji, elimu, afya, barabara na mengineyo,” amesema Materi.
Amesema kutokana na maendeleo hayo, wakazi wa Terrat wameshapiga kura zao kwa Rais Samia na kuzihifadhi kwenye rubega wakisubiri mwaka 2025 kuweka kwenye masanduku.