SERIKALI kupitia Taasisi kama
Wakala wa Majengo (TBA),Shirika la Reli Tanzania (TRC), na Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA) wako hatua za mwisho za kukamilisha mkakati wa
namna ya kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza majukumu yao.
Mfano
tu ukikamilika mradi wa SGR ,kutakuwa na vipande vitakavyokuwa
vikifanyiwa ukarabati na sekta binafsi badala ya TRC wenyewe huku
ikielezwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan imekuwa kipaumbele kwa taasisi binafsi hususani katika
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa jijini Arusha na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey
Kasekenya wakati akifungua mkutano wa tatu wa kikanda wa mashauriano na
wadau wa sekta ya ujenzi kwa mwaka 2023 ulioanadaliwa na Bodi ya Usajili
wa Makandarasi jijini Arusha kwa wadau wa ujenzi wa mikoa ya kanda ya
kaskazini.
Aidha imeelezwa makandarasi wa ndani wametakiwa
kutumia wataalam wenye sifa katika kutekeleza shughuli zao, ili kuweza
kukidhi vigezo hitajika na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo na kupunguza matumizi ya wakandarasi wa nje hususani katika
miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB),Mhandishi Joseph
Nyamhanga, ameishukuru Serikali kupuguza matumizi ya force
akaunti,hususani katika majenzi hali ambayo imeamsha tena hari ya
makandarasi wa ndani kufanya kazi.
Nyamhanga amesema ,
“Tunashukuru Serikali kwa kuliona hili,force akaunti sio mbaya,kutumia
katika ujenzi wa darasa moja katika shule inaruhusiwa,lakini kwa miradi
mikubwa tunaomba serikali itumie Makandarasi”.
Wakati huo huo
Msajili wa Bodi ya Makanadarisi Mhandisi Rhoben Nkori ametoa mwito kwa
makandarasi wa ndani kuandika bei halisi ya miradi yao,wakati wa usajili
miradi yao kwa CRB,kwani imebainika baadhi ya makandarasi kuandika
gharama ndogo ya miradi yao tofauti na mikataba waliyoingia.
“Tumebaini
baadhi ya makandarasi kuandika gharama ndogo ya miradi yao,wakati wa
kutembelea shughuli zao tunakuta gharama ya mradi ni tofauti na
aliyosajilia mradi kwenye mfumo,hii ni kinyume cha sheria”.amesema
Mhandisi Nkori.
Mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha
makandarasi kutoka mikoa sita ya kaskaskazini na mikoa jirani ,ikiwemo
mkoa wa Arusha,Kilimanjaro,Manyara,Tanga,Singida na Dodoma,ambapo
makandarasi watajadili na kuweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta
ya makandarasi nchini.
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Mhandisi Joseph Nyamhanga.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Mhandisi Rhoben Nkori