Na Victor Masangu,Kibaha
Wanawake bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ya kutokuwa na mitaji kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao mbali mbali za kujipatia kipato ili waweze kujikwamua kimaisha.
Katika kuliona hilo Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Selina Koka ameamua kuchangia kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wa uwt kata ya maili moja na kata ya tumbi ikiwa kama ni msingi wa kuanza shughuli za wajasiriamali.
Mama Koka ambaye pia ni mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha mji amesema nia yake kubwa ni kuhakikisha anawafungulia akaunti katika kila kata ikiwa sambamba na kuwaingizia fedha kiasi cha laki tano ambazo zitawasaidia katika kujikwamua kiuchumi.
“Kitu kikubwa kwa Upande wangu ni kuendelea kuwasaidia kwa hali na mali wanawake wote wa uwt katika Jimbo la Kibaha mjini na nimetoa laki tano kwa kata 13 hadi sasa na kesho nitatoa kata ya visiga na nitakuwa nimekamilisha zoezi la kutoa kata zote 14,”alisema Selina.
Kadhalika katika hatua nyingine alitoa vifaa vya michezo kwa wanawake wa UWT Kata ya maili moja vikiwemo mipira pamoja na jezi 14 ili kuanzisha timu za mchezo wa netiboli katika kila kata zote 14 za kibaha mjini.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mji Elina Mgonja amewataka wanawake kuweka misingi ya kuwa wazalendo na kwamba wanatakiwa kuweka mipango ya kuongeza idadi ya wanachama.
Mwenyekiti huyo alibainisha kwamba lengo kubwa la kufanya ziara hiyo ni kuzungumza na viongozi mbali mbali pamoja na kuangalia uhai wa jumuiya katika ngazi zote kuanzia kwenye matawi.