Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amemuaga Balozi wa Jamhuri ya Rwanda nchini Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba, baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.
Akiongea wakati wa hafla ya kumuaga Balozi Karamba iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Dkt. Tax amempongeza Balozi Karamba kwa kumaliza muda wake wa uwakilishi salama na kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kukuza na kudumisha uhusiano mzuri na wa kindugu baina ya Tanzania na Rwanda katika kipindi chake cha uwakilishi nchini.
Aidha, Mhe. Tax ameeleza kwamba, wakati wa Uwakilishi wake, Balozi Karamba amechangia Kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano wa Tanzania na Rwanda katika maeneo mbalimbali ikiwemo, biashara na Uwekezaji, Nishati, uchukuzi na ujenzi, na yapo maeneo ambayo nchi hizi mbili zitaendelea kushirikiana kwa ukaribu na maeneo mengine Tanzania itaendelea kubadilishana uzoefu na Rwanda.
Naye, Mhe. Balozi Karamba ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.
Mhe. Balozi ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili na kupongeza hatua mbalimbali ambazo Tanzania imeendelea kuzichukua katika kuimarisha mahusiano hayo.