Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa darasa la awali katika shule ya msingi Kipapa Halmashauri ya wilaya Mbinga baada ya kuzindua vyumba viwili vya madarasa kwa ajili ya elimu ya awali,kushoto Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas akipanda mti wa kivuli katika shule ya msingi Kipapa wilayani Mbinga.
Na Muhidin Amri,
Mbinga
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezindua madarasa mawili ya awali yaliyojengwa katika shule ya Msingi Kipapa tarafa ya Hagati Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni muendelezo wa shughuli zinazofanyika kwenye maeneo mbalimbali Wilayani Mbinga katika wiki hii ya maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Akitoa taarifa ya ujenzi kwa Mkuu wa Mkoa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kipapa Saulo Komba amesema, mradi huo unaojumuisha ujenzi wa madarasa mawili, matundu 6 ya vyoo, meza na viti pamoja na mfumo wa maji hadi kukamilika kwake umegharimu shilingi Milioni 57.9 ambapo utekelezaji wake ulianza Agosti 2022 na kukamilika Novemba 2022.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas, amepongeza juhudi zilizofanywa na uongozi wa shule, Halamashauri ya kijiji cha Mpapa na Wilaya katika kusimamia kikamilifu mradi huo.
Kanal Laban ametoa wito kwa wanafunzi, walimu na jamii nzima kuzingatia ulinzi na utunzaji wa miundombinu ya shule hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa, amekemea kukithiri kwa matukio yanayosababishwa na mmomonyoko wa maadili ikiwemo ubakaji,unyanyasaji wa kijinsia na ulawiti hasa kwa watoto wa kiume.
Mkuu wa mkoa amesisitiza kuwa, suala la malezi ya watoto linapaswa kuwa jukumu la jamii nzima katika kulea na kufatilia maadili ya watoto.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amechangia mifuko 10 ya saruji katika kuunga mkono jitihada za wananchi wa kijiji cha Kipapa kwa kuanzisha ujenzi wa darasa kwa nguvu zao ambalo bado lipo hatua ya awali ya ujenzi wake huku pia akishiriki zoezi la upandaji wa miti kwenye shule hiyo ambapo miti 400 imepandwa.