Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Africa la nchini Marekani kumfanyia upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cath lab mgonjwa mwenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu hayo leo jijini Dar es Salaam. Wagonjwa 15 wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Wataalamu wa afya ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimfanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Cardiography – ECHO) mgonjwa ambaye ana matatizo za mfumo wa umeme wa moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu hayo leo jijini Dar es Salaam. Wagonjwa 15 wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Wataalamu wa afya ya Taasisi Ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani wakiandaa vifaa kwa ajili ya kumfanyia upasuaji wa moyo mgonjwa ambaye ana matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu hayo leo jijini Dar es Salaam. Wagonjwa 15 wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Picha na: JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa kiasi cha shilingi milioni 493 ambazo Serikali ingetumia kama wagonjwa 15 wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Peter Kisenge alisema katika kambi hiyo maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani wameweza kuwafanyia upasuaji wagonjwa ambao walihitaji kurekebishiwa mfumo wa umeme wa moyo kwa ufasaha wa hali ya juu.
Dkt. Kisenge alisema pamoja na wataalam hao kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa pia wametoa mafunzo kwa wataalam wa afya wa JKCI hivyo kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo katika Taasisi hiyo.
“Gharama za matibabu za wagonjwa hawa 15 ni shilingi milioni 253 lakini kama wagonjwa hawa wangeenga kutibiwa nje ya nchi wangetumia shilingi milioni 746. Serikali imeweza kuokoa kiasi cha shilingi milioni 493 kwa wagonjwa hawa kutibiwa ndani ya nchi”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge amewaomba wananchi kukata bima za afya ili kupata huduma za matibabu kwa urahisi pale wanapohitaji huduma hizo kwani matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo ni ya gharama.
“Bima ya afya kwa wote itakapoanzishwa nawaomba wananchi mjitokeze ili mpate fursa ya kupata matibabu kwa urahisi kwani ugonjwa utokea wakati wowote na unaweza kukukuta hauna fedha lakini unapokuwa na bima ya afya itakupa urahisi wa kupata matibabu”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa JKCI Yona Gandye alisema katika kambi hiyo wamewatibia wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yalikuwa chini na wengine mapigo yao ya moyo yalikuwa juu sana .
“Tumewatibia wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yanazalishwa kwa kiwango cha chini sana kwa kuwawekea kifaa kisaidizi cha moyo ambacho kinausaidia moyo kufanya kazi vizuri (pace maker) na wale ambao mapigo yao ya moyo yako juu sana tumeyapunguza kwa kutumia mtambo wa Carto 3”, alisema Dkt. Gandye.
“Katika kambi hii wagonjwa sita walikuwa na matatizo katika mfumo wa uzalishaji wa mapigo ya moyo hivyo mioyo yao kwenda haraka sana na kusababisha moyo kutanuka, wagonjwa wawili walibadilishiwa vifaa visaidizi vya moyo vilivuokuwa vimeisha muda wake”,
“Wagonjwa watano ambao mapigo yao ya moyo yalikuwa chini waliwekewa vifaa visaidizi vya moyo (pace maker) hawa mapigo yao ya moyo yalikuwa yapo chini sana, na wagonjwa wengine wawili mapigo yao ya moyo upande wa kushoto yalikuwa hayazalishi umeme wa moyo vizuri”, alisema Dkt. Gandye.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani Prof. Matthew Sackett alisema wamekuja katika Taasisi hiyo kuboresha huduma za matibabu kwa wataalam wa afya wa JKCI kuifanya Taasisi hiyo kuwa kituo cha kibingwa cha matibabu ya moyo kusini mwa jangwa la Sahara.
“Nchi nyingi za ulaya hutoa matibabu haya, tukaona ni vyema tusogeze huduma hizi na nchi za Afrika ili nao waweze kupata huduma kwa urahisi na kwa karibu ndio maana tumeendelea kushirikiana na Taasisi hii kuboresha huduma za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo”, alisema Prof. Sackett