Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imetajwa kuwa ni miongoni mwa Hifadhi inayonufaika na Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) ambapo kwa sasa ndege zaidi ya tisa za watalii zimekuwa zikitua kutokana na kukarabatiwa kwa kiwanja cha ndege cha Kikoboko hali iliyopelekea kuwepo kwa usalama wa kutosha kwa watalii.
Mhifadhi Mkuu wa Idara ya Ujirani Mwema na Uhusiano, David Kadomo ametoa kauli hiyo leo April 27, 2023 wakati akielezea jinsi Mradi wa REGROW unavyoendelea kuleta mapinduzi makubwa katika Hifadhi hiyo iliyopo Mkoani Morogoro.
Amesema mradi wa REGROW umeinufaisha sana Hifadhi hiyo ambapo REGROW imeweza kutoa vitendea kazi ikiwemo mitambo na magari kwa ajili ya kukarabati uwanja huo wa ndege na kwamba hali hiyo imepelekea ndege nyingi kutua huku akisisitiza kuwa kabla ya hapo ndege nyingi zilikuwa zikikwama katika uwanja huo.
Amefafanua kuwa Mradi wa REGROW umechangia idadi ya ndege zinazotua kwa siku katika Hifadhi hiyo kuongezeka maradufu kutoka wastani wa ndege tatu kwa siku hadi ndege tisa kwa siku ambapo amesema watalii wengi wanaotembelea Hifadhi hiyo wanatokea Zanzibar kwa njia ya ndege.
Hata hivyo,Mhifadhi Mkuu Kadomo amesema idadi hiyo ya watalii mbali ya kuchangiwa na kuimarika kwa miundombinu katika Hifadhi hiyo pia Filamu ya The Royal Tour imechangia kwa kiasi kikubwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi hiyo.
Amebainisha kuwa kutokana na kukarabatiwa kwa uwanja huo hata baadhi ya ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba watalii zaidi ya 42 zimekuwa zikitua ambapo mwanzo ndege ndogo tu zenye kubeba watalii 12 ndizo zilikuwa zikiweza kutua katika uwanja huo .
Kufuatia kuongeza kwa idadi hiyo ya ndege Mhifadhi Mkuu Kadomo amesema idadi ya watalii pia imeongeza kutoka watalii elfu 59 hadi watalii elfu 90.
Amefafanua kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi hivi sasa imepokea jumla ya watalii elfu 90 ambapo kabla kuboreshwa kwa miundombinu hiyo walikuwa wakipokea watalii elfu 59 tu.
Kufuatia takwimu hizo, Bw.Kadomo amesema hadi ifikapo mwezi Juni mwaka huu Hifadhi hiyo inatarajia kupokea jumla ya watalii 100,000 na mapato Shilingi Bil.3.9 yatokanayo na watalii.
Ameongeza kuwa “Hatukuwahi kupata wataliii kama hao kabla ya Mradi wa REGROW kukarabati miundombinu ya watalii katika Hifadhi yetu ya Mikumi hiyo tunaushukuru sana Mradi huu “
Mradi wa REGROW ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza Sekta ya Utalii katika Mikoa ya Kusini. Mradi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia.