MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt.Amos Nungu, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo Aprili 27,2023 jijini Dodoma kwenye banda la Tume hiyo katika Maonesho ya wiki ya ubunifu 2023 yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia yanayofanyika uwanja wa Jamhuri Dodoma.
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt.Amos Nungu, akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 27,2023 jijini Dodoma kwenye banda la Tume hiyo katika Maonesho ya wiki ya ubunifu 2023 yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia yanayofanyika uwanja wa Jamhuri Dodoma.
WANANACHI wakipata maelezo mara baada ya kutembelea banda la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) leo Aprili 27,2023 jijini Dodoma kwenye banda la Tume hiyo katika Maonesho ya wiki ya ubunifu 2023 yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia yanayofanyika uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt.Amos Nungu,amewataka vijana wa kitanzania kutambua na kuamini juu ya ubunifu unaofanywa nchini badala ya kusifia bunifu za nje ya nchi.
Hayo ameyasema leo Aprili 27,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la Tume hiyo katika Maonesho ya wiki ya ubunifu 2023 yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia yanayofanyika uwanja wa Jamhuri Dodoma.
“Kwa sasa serikali kupitia COSTECH imeweza kuwaweka sokoni vijana wengi ambao wameonekana kuwa wabunifu kwa kuwapatia vibali vya kuwaendeleza na kuwajengea uwezo wa kiuchuni jambo ambalo linaendelea kutoa hamasa katika jamii”amesema Dkt.Nungu
Hata hivyo amesema kuwa Vijana wengi ambao wanajitokeza kwa kujitambulisha kuhusu ubunifu walionao wamekuwa wakisaidiwa kwa kuendelezwa au kuunganishwa katika mashirika mbalimbali nchini.
Aidha ametoa wito kwa vijana kuacha kukopi bunifu za wengine na kubuni kitu chako cha utofauti ili uweze kuweka rekodi ya kipekee kama kijana kwa kuwa wa kwanza kubuni bunifu ya kipekee na yenye tija na kuleta ushawishi kwenye jamii.
Dkt.Nungu amewataka watanzania kuziamini na kuzitumia bunifu zinabuniwa na vijana wa kitanzania ikiwemo kuzinunua na kurejesha mrejesho kwa wabunifu kama sehemu ya kuziboresha.
“Sisi COSTECH kwa mfano katika MAKISATU yaliyopita kuna kijana alibuni gari ya kutumia mfumo wa umeme lakini alivyokuja kwetu tukabaini mapungufu na tukamdhamini kwa kumpatia kiasi cha shilingi milioni 10 ili akaboreshe yale mapungufu,”ameeleza Dkt.Nungu
Kuhusu wabunifu ambao wanabuni vifaa ambavyo ni hatarishi kama vile gobore au bunduki amesema kuwa wanatakiwa kuwasiliana na COSTECH kabla ya kuingia sokoni kwa kuuza bidhaa hizo.
”Serikali kazi yake kubwa ni kuwawezesha na kuwajengea uwezo wabunifu ambao wanaonekana kubuni vifaa hatarishi kwa kulinda usalama wa nchi na siyo kazi ya serikali kuwakamata na kuwaweka ndani.”amesema