Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri mkuu Kazi,Vijana, Ajira,na Wenye ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama Mahala pa kazi kitaifa yatakayofanyika mkoani Morogoro.
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Usalama na afya mahala pa kazi (OSHA) Bi.Khadija Mwenda,akizungumza kuelekea maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama Mahala pa kazi kitaifa yatakayofanyika mkoani Morogoro.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA)Tumaini Nyamhokya,akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama Mahala pa kazi kitaifa yatakayofanyika mkoani Morogoro.
MWAKILISHI wa Shirika la kazi Duniani (ILO) Bi. Getrude Sima ,akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama Mahala pa kazi kitaifa yatakayofanyika mkoani Morogoro.
Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri mkuu Kazi,Vijana, Ajira,na Wenye ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama Mahala pa kazi kitaifa yatakayofanyika mkoani Morogoro.
Na.Alex Sonna-DODOMA
TAKWIMU za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zilizotolewa katika kipindi cha mwaka 2022, zinaonyesha kuwa watu milioni 2.9 walipoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Pia, zaidi ya wafanyakazi milioni 402, huumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu.
Hayo yamesemwa leo Aprili 26,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri mkuu Kazi,Vijana, Ajira,na Wenye ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama Mahala pa kazi kitaifa yatakayofanyika mkoani Morogoro.
Prof.Joyce Ndalichako amesema Kwa upande wa Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249. Katika ajali hizo, vifo vilikuwa 217.
Aidha amesema kuwa takwimu hizo ni kubwa na zinaathiri utendaji kwa kuwa zinasababisha upotevu wa maisha ya wafanyakazi na pia kuathiri shughuli wakati walioumia wakiendelea kupata
matibabu.
“Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kwamba suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi linahitaji jitihada za makusudi katika kukabiliana nalo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa kulinda nguvu kazi ya Taifa.
“Tunapoelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa Kazi tarehe 28 Aprili 2023, serikali kwa kushirikiana na wadau wetu wa utatu tunaendesha kampeni maalum ya uhamasishaji kupitia shughuli za mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye
ulemavu”amesema
Prof.Ndalichako amesema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa Mkoani Morogoro katika viwanja vya Tumbaku Aprili 28,2023
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),Tumaini Nyamhokya ameiomba serikali kuweka sheria kali zilizopo ili ziweze kuwabana waajiri katika kuhakikisha kunakuwa na usalama mahali pa kazi.
Mwakilishi wa Shirika la kazi Duniani (ILO), Bi Getrude Sima amesema wataendelea kushirkiana na serikali ya Tanzania
Siku ya usalama mahala pa kazi duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1996 nchini Marekani ambapo waathirika na watu walioumia na kupoteza maisha wakiwa kazini hukumbukwa ambapo kwa Tanzania ilianza kuadhimishwa mwaka 2004.
Kauli mbiu yam waka huu inasema Mazingira salama na afya kazini ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi.