Mkuu Wa Wilaya ya Momba, Fakii Lalandala akizungumza na wadau wa Bodi ya Nafaka na mazao mchanganyiko katika kikao kilichofanyika Tunduma.
Sehemu ya wadau wakimsikiliza Mkuu Wa Wilaya ya Momba, Fakii Lalandala (hayupo pichani) wakati akizungumza na wadau wa Bodi ya Nafaka na mazao mchanganyiko katika kikao kilichofanyika Tunduma.
Mkuu Wa Wilaya ya Momba, Fakii Lalandala akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Bodi ya Nafaka na mazao mchanganyiko katika kikao kilichofanyika Tunduma.
NA MWANDISHI WETU,TUNDUMA
MKUU wa Wilaya ya Momba Fakii Lalandala ameahidi kutoa Hekali 200 za ardhi bure kwaajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata mazao kitakacho milikiwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alisema endapo CPB itajenga kiwanda hicho katika eneo hilo itasaidia kuinua Uchumi wa Wananchi ambao ni wakulima wa ukanda huo kwani watapata soko la uhakika la kuuza mazao yao.
Akizungumza jana alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa CPB kilichofanyika Tunduma Wilaya ya Momba, Mkuu huyo wa Wilaya alisema amefurahi sana kukutana na Bodi hiyo ya Nafaka inayofanya biashara ya kununua mazao na kuyachakata kwani mazao hayo yanalimwa kwa wingi Wilayani humo.
‘’Nasema CPB hapa mmefika, kuna eneo la hekari mia mbili nawapa bure mje kuwekeza kiwanda hapa, naamini uwekezaji huo utainua Uchumi wa mtu mojamoja na hata Serikali kwa Ujumla’’, alisema Mkuu huyo wa Wilaya Momba.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema mazao yanayolimwa kwa wingi Wilayani hapo ni pamoja na Mahindi, Mpunga na Maharage hivyo anaamini uwekezaji wa kiwanda Wilayani hapo utasaidia kuinua Uchumi wa Wakulima kwani wakulima hao watapata soko la uhakika kwa na kwa bei ya soko.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya CPB Salum Awadh alisema yuko tayari kutuma watu wakafanye tathmini katika eneo hilo kama linafaa kujenga kiwanda cha kuchakata mazao.
‘’Natoa agizo viongozi wa CPB wataenda kuliangalia eneo hilo na kufanya tathmini tukijiridhisha tutakuja kujenga Kiwanda cha kuchakata mazao Wilayani Momba’’, alisema Awadh.
Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha CPB imetenga Sh. Billioni 100 kwaajili ya kununua mazao na uwekezaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Awadh alisema wataendelea kujenga viwanda sehemu mbalimbali ili waweze kupata malighafi nyingi na kuzalisha kwa wingi kwaajili ya kufanya biashara ya mazao ndani na nje ya nchi.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Bodi amewataka wakulima na wafanyabiashara wa mazao kutumia fursa hiyo kuuza mazao yao CPB hivyo aliwataka mamneja wa cpb kuingia mikataba na wakulima ili wapate soko la uhakika.
Hata hivyo Awadh alisema tayari CPB ina viwanda vya kuchakata mazao katika Mikoa ya Dodoma, Iringa, Arusha, Mwanza,Dar es Salaam na wanatarajia kujenga kiwanda vingine Handeni Tanga.
CPB ni Shirikia la Kiserikali linalofanya biashara ya kuomgezea thamani ya mazao kwani baada ya kununua mazao kutoka wakulima wanachakata katika viwanda vyao na kuuza bidhaa hizo ndani nan je ya nchi.
CPB itafanya vikao vya wadau katika katika kanda zao zilizopo Kanda ya Kaskazini Arusha, Kanda ya Ziwa Mwanza na Kanda ya Pwani Dar es Salaam.