Alavuya Mtalima wa Wizara ya Mambo ya Ndani akimaliza wa kwanza katika mbio za baiskeli kilometa 25 kwa wanawake zilizoanzia eneo la Lugono na kumalizikia eneo la Mafiga stendi katika mchezo wa Kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani Morogoro.
James Shigela wa Wizara ya Mambo ya Ndani akishangilia baada ya kutwaa ubingwa wa mbio za baiskeli kwa wanaume alipomaliza Kilometa 35 zilizoanzia eneo la Melela Mlandizi na kumalizikia Mafiga Stendi katika michezo ya Kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani Morogoro.
Timu ya Ofisi ya Rais Ikulu (kushoto) wakivutana na Wizara ya Kilimo katika mchezo wa Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Ikulu wameshinda kwa mivuto 2-0.
Timu ya wakawake ya Mahakama (kushoto) wakiwavuta Ofisi ya Waziri Mkuu Sera kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Timu ya Hazina (kulia) ikivutwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa mivuto 2-0 ikiwa ni moja ya michezo ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Timu ya wanaume ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) (kushoto) wakiwavuta ndugu zao Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa Kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani Morogoro.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WIZARA ya Mambo ya Ndani leo imekuwa mwiba mkali kwa washiriki wa michezo ya Kombe la Mei Mosi kwa kutwaa ubingwa wa wanawake na wanaume katika mchezo wa baiskeli uliofanyika mkoani hapa.
Mbio hizo za baiskeli wanawake zilikuwa kilometa 25 zilianzia eneo la Lugono, wakati za wanaume zilikuwa kilometa 35 zilianzia eneo la Melela Mlandizi na zote zilimalizikia eneo la Mafiga Stendi.
Bingwa wa wanawake, Alavuye Mtalima alitumia dakika 29:35.12, akifuatiwa na Scolastica Hamis kwa dakika 30:37.20 na wa tatu ni Bernadetha Petro wa Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC); wakati kwa wanaume bingwa ni James Shigela wa Wizara ya Mambo ya Ndani ametumia dakika 57:43.00; akifuatiwa na Steve Sanga wa Taasisi ya Saratani Ocean Roads alitumia dakika 58:45.00 na mshindi wa tatu ni Hassan Ligoneko wa Wizara ya Afya alitumia saa 1:07.00. Washiriki wote kwa wanawake na wanaume walikuwa tisa kila mmoja.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume timu ya Ofisi ya Rais Ikulu waliwavuta Wizara ya Kilimo kwa 2-0; huku Wizara ya Mambo ya Ndani waliwavuta Taasisi ya Saratani Ocean Roads kwa 2-0; TPDC waliwavuta Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa 2-0, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) waliwavuta jamaa zao Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa 2-0; nazo Mahakama na Wizara ya Afya zilipata ushindi wa chee baada ya wapinzani wao RAS Dodoma na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kushindwa kuingiza timu.
Kwa upande wa wanawake timu ya Mahakama waliwavuta Ofisi ya Waziri Mkuu Sera kwa 2-0; huku TANROADS waliwashinda Hazina kwa 2-0; nayo Wizara ya Afya waliwashinda Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa 2-0; wakati Wizara ya Maliasili na Utalii walipata ushindi wa chee baada ya TAMISEMI kuingia mitini.
Katika mchezo wa mpira wa wavu kwa wanaume Wizara ya Maliasili na Utalii waliwashinda Moro Sec kwa seti 2-0; nayo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) waliwachapa RAS Dodoma kwa seti 2-0; na Sekta ya Uchukuzi waliwaadhibu Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa seti 2-0; wakati kwa wanawake RAS Dodoma waliwachapa TPDC kwa 2-1 na Sekta ya Uchukuzi waliwapiga Moro DC kwa seti 2-1.
Michuano hii inaendelea kesho Jumatatu tarehe 24 April, 2023 kwa michezo ya netiboli hatua ya robo fainali, mpira wa wavu na riadha.