WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Anjelina Mabula, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Aprili 21,2023 jijini Dodoma kuhusu maboresho mbalimbali yaliyofanyika kuhusu ulipaji wa kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine ya Sekta ya Ardhi.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Anjelina Mabula,amesema Wizara imefanya maboresho katika mfumo mzima wa utunzaji kumbukumbu za ardhi, utozaji wa kodi na utoaji wa huduma za Sekta ya Ardhi.
Waziri Mabula ameyasema hayo leo Aprili 21,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maboresho mbalimbali yaliyofanyika kuhusu ulipaji wa kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine ya Sekta ya Ardhi.
Amesema maboresho yaliyofanyika kwenye mifumo unaowezesha wamiliki wa ardhi kupokea ujumbe kupitia simu za mkononi.
Dkt.Mabula amesema katika msamaha wa kodi ya ardhi uliotolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan baadhi ya wananchi walishindwa kunufaika ikiwemo taratibu zinazowataka kufika katika ofisi za ardhi ili kukadiria na kujua deni la msingi na riba itakayosamehewa.
“Miongoni mwa maboresha makubwa yaliyofanyika katika kipindi hiki kifupi ni kuboresha mifumo ili iweze kutuma ujumbe mfupi wa maandishi unatumwa kwa wadaiwa wote kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati kupitia simu za viganjani,”amesema Dkt.Mabula
Hata hivyo amesema kuwa hadi sasa zaidi ya jumbe 84,000 za simu zimetumwa kwa wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi zikiwa na deni la msingi kiasi cha takribani Sh.Bilioni 115 ambazo zinatarajiwa kukusanywa katika Mikoa 25.
Amesema kuwa Mkoa uliobaki ambao ni Dar es Salaam zoezi hili linaendelea na ifikapo tarehe 30 Aprili, 2023 wamiliki wa ardhi katika Mikoa yote ya Tanzania Bara watakuwa wametumiwa jumbe kupitia simu za mkononi kuhusiana na madai ya kodi ya pango la ardhi.
“Wananchi wote wakiona ujumbe katika simu ukianza na neno “ARDHI” wajue ni jumbe sahihi na zinatoka Wizara ya Ardhi zikiwakumbusha kulipa kodi kwa wakati ili wanufaike na msamaha uliotolewa na Rais Samia ambao mwisho ni Aprili 30, 2023,”amesema.
Hata hivyo amesema kuwa Wizara itachukua hatua za kisheria ikiwamo kuwafikisha mahakamani wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi ili kufidia kodi husika au kupendekeza ubatilisho wa milki kama masharti ya umiliki yanavyojielekeza.
“Natoa wito kwa wamiliki wa ardhi wenye madeni kuchangamkia nafuu iliyotolewa na Rais ya kulipa madeni yao ya msingi ili wasemehewe riba ndani ya muda uliotolewa,”amesema