Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na kamati ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Mei Mosi alipokutana nao katika ukumbi wa Mbaraka Mwinshehe, Mkoani Morogoro.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe ya Siku ya Wafanyakazi walifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) walipokutana kwa lengo la kupokea taarifa na kukagua maandalizi hayo.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya (kulia) akieleza jambo wakati wa kikao hicho. Katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa akitoa taarifa ya hatua za maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Mei Mosi wakati wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mbaraka Mwinshehe, Mkoani Morogoro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akijadili jambo na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya (kulia) wakati wa kikao hicho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (katikati) pamoja na wajumbe wa kamati wakiwa katika ukaguzi wa maandalizi ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro. Wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa. Wa pili kutoka kulia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
Na.OWM – KVAU: MOROGORO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amekagua maandalizi ya sherehe za Mei Mosi na kueleza ameridhishwa na hatua zilizofikiwa.
Amesema hayo Aprili 20, 2023 baada ya kupokea taarifa ya kamati ya maandalizi walipokutana kwa lengo la kujadili na kupanga mipango mbalimbali kuelekea kilele cha sherehe hizo zinazotarajiwa kuadhimishwa katika uwanja wa Jamhuri, Mkoani Morogoro.
Aidha, Waziri Ndalichako amepongeza kamati ya mkoa kwa kushirikiana na ofisi yake pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ili kufanikisha sherehe hiyo.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri, hakika hatua iliyofikiwa katika maandalizi inaridhisha,” amesema
“Nipongeze Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kwa namna wanavyoratibu shughuli hii na tunawaunga mkono kwa kuwa tunatambua umuhimu wa wafanyakazi katika kutekeleza malengo ya Serikali,”
Sambamba na hayo amehamasisha wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 1 Mei, 2021.
Prof. Ndalichako pia ametumia fursa hiyo kushukuru wadhamini na wadau mbalimbali kwa michango yao ambayo itasaidia kufanikisha shughuli hiyo. Vilevile amewataka wanakamati kuendelea kusimamia shughuli zinazofanyika uwanjani hapo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa amesema kuwa mkoa huo umejipanga vizuri katika kufanikisha sherehe hiyo muhimu kwa kuzingatia mambo matano ya msingi ikiwemo kuratibu suala la rasilimali fedha za maandalizi, kuandaa uwanja wenye hadhi, kuhamasisha wananchi kushiriki kwa shamrashamra kuelekea siku hiyo na kutangaza maadhimisho hayo ya siku ya wafanyakazi.
Maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi 2023 yataadhimishwa kitaifa katika mkoa wa Morogoro, yakiwa na kauli mbiu isemayo “Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi. Wakati ni Sasa.”