Tunapoelekea kipindi hiki cha kusherekea sikukuu ya Eid El Fitri Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wananchi wote kuwa makini na kusherekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu pasipo vitendo au viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani
Ikumbukwe kuwa wananchi wote katika Mkoa wa Mwanza wenye imani ya kiislamu na hata madhehebu mengine kutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe, wakati mwingine baadhi ya watu wasio wastaarabu wanaweza kutumia kipindi hicho cha sikukuu kwa kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko ya watu maeneo mbalimbali.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linapenda kuwatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Mwanza na kuwahakikishia kwamba askari wake wamejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wanasherekea sikukuu za Eid El Fitr kwa amani na utulivu. Ulinzi utaimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya swala ya Iddi, fukwe za ziwa, sehemu za starehe na maeneo mengine yote. Aidha, tunapenda kuwatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki kuepuka kwenda mwendo kasi au kutumia vilevi wakati wa kuendesha vyombo vya moto.
Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu
kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunawashukuru wale wote ambao tayari wamefunga kamera zao za CCTV katika maeneo ya starehe, hususani yale yanayokuwa na mikusanyiko ya watu, yakiwemo maduka, hoteli, supermarket, malls, na maeneo ya benki. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunaendelea kuwasisitza wale ambao hawajaweka kamera hizo, kuweka ili kuweza kubaini wahalifu na
hata kurahisisha ukamataji endapo uharifu utatokea.
Vilevile, wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao. Hivyo jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza hatutaruhusu disko toto katika maeneo mbalimbali badala yake wazazi wanashauiriwa kuwapeleka watoto wao katika maeneo ya wazi ambapo kutakuwa na ulinzi na doria za kutosha za askari wa Jeshi la Polisi tukishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Aidha, wananchi wachukue tahadhari za kutosha watokapotoka kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na watoe taarifa kwa majirani zao na pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa haraka kwenye vituo vya Polisi vilivyo karibu nao au kwa askari wetu wa doria, wanaofanya doria katika mitaa, kwa wakuu wa polisi wa wilaya, maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi au kwa Kmanda wa Polisi Mkoa ambaye namba zake za mawasiliano ni 0715- 009949 na 0739-009949.
Jeshi la Polisi mkoa Wa Mwanza tunawatakia Eid Mubaraka wakazi wote wa Mkoa wa Mwanza na tunawatakia washerekee sikukuu hizo kwa amani na utulivu.
Tarehe 16.04.2023 muda wa saa 21:45 usiku, huko maeneo ya Bwiru Msikitini, kata ya Pasiansi, Tarafa na Wilaya ya Ilemela, kuliripotiwa taarifa ya Emmanuel Nyambera, miaka 40, mfanyabiahashara na mkazi wa Bwiru Msikitini aliyejipiga risasi kifuani upande wa kushoto na kupelekea kifo chake. Emmanuel Nyambera alikuwa akimiliki Pistor yenye namba za usajili TZCAR80190 Model namba 79 KCAL 38 aina ya charter ambayo inauwezo wa kuchukua risasi tisa (9) na ndio aliyotumia kujifyatulia risasi kifuani.
Chanzo cha tukio hilo ni migogoro ya kifamilia iliyotokana na mgawanyo wa mali za familia ambapo Emmanuel Nyambera alikua hajalidhia jambo lililompelekea kuwa na msongo wa mawazo na kupelekea kujipiga risasi. Mwili wa Emmanuel umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Jeshi la Polisi Mkoa Wa Mwanza linaendelea kutoa wito kwa wananchi kutafuta njia nzuri na sahihi ya kutatua migogoro mbalimbali wanayokutana nayo ilikuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.
Imetolewa na;-
Wilbrod Mutafungwa – SACP.
Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.