Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Naibu Mtendaji Mkuu Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda Frederic Ngirabacu wakionesha mkataba wa kutibu wagonjwa wa moyo na kuwajengea uwezo wa kuwatibu wagonjwa wa moyo wataalamu wa afya wa Hospitali hiyo. Mkataba huo umesainiwa jana jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Save a Child’s Heart – SACH la nchini Israel Simon Fisher.
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amelishukuru Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel kwa kuendelea kutoa huduma za upatikanaji wa matibabu ya moyo na ujuzi kwa nchi mbalimbali za Afrika.
Akizungumza baada ya kusaini mikataba ya miaka mitatu wa makubaliano na Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda na Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia wa kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hizo Dkt. Kisenge alisema SACH imekuwa ikiwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo kupata matibabu pamoja na kuwapa ujuzi madaktari wa JKCI.
Dkt. Kisenge alisema SACH ilianza ushirikiano na JKCI tangu mwaka 2015 kwa kuwachukuwa watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo hayakuweza kutibiwa hapa nchini na kuwapeleka Israel kwa ajili ya matibabu ambapo sasa JKCI imekuwa na uwezo wa kutibu magonjwa hayo kwa watoto hivyo kuiunganisha JKCI na nchi za Rwanda na Zambia ili nazo ziweze kupata ujuzi huo.
“Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la Nchini Israel limekuwa likiwahudumia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotoka katika familia duni kuokoa maisha yao na pale walipohitaji kuwapeleka nchini Israel walifanya hivyo kwa upendo”,alisema Dkt. Kisenge.
Akizungumza katika Hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel Simon Fisher alisema hatua iliyofikia hadi Rwanda na Zambia kukubali kusaini mikataba hiyo imetokana na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya SACH na JKCI.
“Leo hii Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inafanya upasuaji mkubwa wa moyo pamoja na upasuaji wa tundu dogo kwa watoto kwa kujitegemea naamini baada ya miaka kadhaa wenzetu wa Rwanda na Zambia nao watakuwa na uwezo huo”, alisema Fisher
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia Dkt. Shumba Chabwela alisema kusaini mkataba wa makubaliano ya kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa nchini Zambia kunaonyesha utimilifu wa ushirikiano uliojengwa na waasisi wa nchi za Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na wa Zambia Keneth Kaunda.
“Kwa niaba ya nchi ya Zambia tunatoa shukrani zetu za dhati kwa kutupa nafasi ya kushirikiana nasi kuwahudumia wagonjwa wetu, kabla hata ya kusaini mkataba huu tayari tulishaanza kuleta wataalam wetu kujifunza katika Taasisi hii”, alisema Dkt. Shumba.
Naye Naibu Mtendaji Mkuu Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda Frederic Ngirabacu alisema ushirikiano katika sekta ya afya na sekta nyingine vinapaswa kufanyika baina ya nchi za Afrika ili kwa pamoja ziweze kukuwa na kuacha kutafuta huduma katika mataifa ya mbali.
“Tumeanza ushirikiano na JKCI wiki hii lakini pia tumefurahi kukuta waafrika wenzetu kutoka Zambia wanashirikiana nao, hii inaonyesha ukomavu katika nchi zetu za Afrika”, alisema Ngirabacu.
Ngirabacu alisema Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la nchini Israel limekuwa likisaidia kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo nchini Rwanda na sasa kuwaunganisha na JKCI ili kuendeleza mashirikiano jambo ambalo hawakulitarajia hapo awali.
Mwihso