Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe ameshiriki katika Futari na baadhi ya wakazi wa wilaya ya Bukombe mkoani Geita Aprili 18, 2023.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Biteko amewataka wananchi wa Bukombe kuungana katika dini zao ili kudumisha amani na mshikamano walionao katika wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
“Tufanye siasa lakini tusithubutu hata kidogo kuvunja mwiko wa mshikamano wetu kama wananchi wa Bukombe, tupo na mchanganyiko mwingi na dini mbalimbali tusizitumie dini zetu kugawanyika,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka wananchi wa Bukombe kupendana ili kuendelea kuijenga Bukombe ya sasa na baadaye ili kuleta maendeleo na kudumisha amani.
Naye, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hassan Kabeke amewataka Watanzania kumuombea Rais Samia ili aendelee kuliongoza vyema taifa letu. Pia amewataka kuungana kama taifa kuliombea ili kupinga matendo maovu ikiwemo ushoga na usagaji katika nchi hii.
Futari hiyo iliyoandaliwa na Dkt. Biteko imehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Viongozi mbalimbali wa dini, Viongozi wa Serikali, Wabunge, Madiwani pamoja na wananchi wa Bukombe.