Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof.Joyce Ndalichako,akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2023/24, leo Aprili 13,2023 jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Joyce Ndalichako akiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu, Mhe.Jenista Mhagama(kulia) na Mbunge wa Viti maalum, Khadija Taya (katikati) baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Joyce Ndalichako akiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu, Mhe.Jenista Mhagama, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Mhe.Patrobas Katambi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt.Angelina Mabula baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Patrobas Katambi akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF, NSSF na WCF baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Joyce Ndalichako wakipongeza na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof.Jamal Katundu baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2023/24
Mawaziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Watendaji wa Ofisi hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof.Joyce Ndalichako, amesema ulipaji wa mafao ya wastaafu umeimarika kwa kiwango kikubwa.
Akichangia Aprili 13, 2023, hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2023/24, amesema changamoto zilizokuwa zinasababisha wastaafu wasilipwe kwa wakati na serikali ya awamu ya sita imezifanyia kazi.
“Changamoto kubwa iliyokuwepo ilikuwa ni ukwasi kulikuwa na deni la wafanyakazi waliorithiwa kutoka kwenye mfuko wa PSPF ambao wafanyakazi kabla yam waka 1999 walikuwa hawachangii kwa hiyo serikali ilipowaingiza kwenye mfuko iliahidi kuwalipia michango kiasi cha Sh.Trilioni 4.6 na serikali ya awamu ya sita tayari imetoa Sh.Trilioni 2.17,”amesema.
Amelihakikishia Bunge kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii imeimarisha mifumo yake ya ulipaji mafao kwa wastaafu na wanalipa kwa wakati ndani ya muda uliowekwa kisheria.
Kadhalika, Mhe.Ndalichako amefafanua kanuni ya kukokotoa mafao kwa watumishi wa umma ambayo ilianza kutumika Julai mosi, 2022 imetokana na sheria namba mbili yam waka 2018 ya mfuko wa hifadhi ya jamii ambayo imeanzisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) iliyounganisha mifuko minne ya GEPF, LAPF, PPF na PSPF.
“Kabla ya kuunganisha mifuko ilikuwa na kanuni tofauti za ulipaji wa mafao, Mfuko wa GEPF, PPF ulikuwa unalipa mafao ya mkupuo ya asilimia 25 na Mfuko wa LAPF na PSPF ulikuwa unalipa mafao ya mkupuo ya asilimia 50, lakini mfuko wa NSSF ulikuwa unatoa mafao ya mkupuo ya asilimia 25,”amesema.
Amebainisha kuwa baada ya mifuko kuunganishwa kulikuwa na uwianishaji kanuni na mwaka 2018 ziliundwa kanuni za kutekeleza sheria hiyo ambazo ziliweka watumishi wote walipwe mafao ya mkupuo ya asilimia 25.
“Kanuni ilivyoanza kutumika wale waliokuwa wanalipwa asilimia 50 hadi 25 waliona wameshushwa pa kubwa na kukawa na malalamiko, na serikali ilisitisha na kukaa na wafanyakazi na ikaja na kanuni ya asilimia 33, Kanuni hii lengo lake ilitaka kuwakutanisha katikati wale waliokuwa wanapata asilimia 50 na wale wa asilimia 25,”amesema.
Amesema kanuni ya asilimia 33 imeongeza mafao ya mkupuo kwa wanachama milioni 1,364, 050 sawa na asilimia 81 ya wanachama wote waliokuwa wanapata asilimia 25.
“Watumishi kwenye taasisi zote za umma mafao yenu yameongezeka kutoka asilimia 25 hadi 33 na watumishi wa sekta binafsi kupitia kanuni hiyo mafao ya mkupuo yameongezeka.Katika kanuni hii kuna wafanyakazi 326,137 sawa na asilimia 19 ndio hao waliokuwa na asilimia 50 wamekuja kwenye asilimia 33 lakini mafao yao ya pensheni kwa mwezi yameongezeka kutoka asilimia 50 hadi 67,”amesema.
Aidha, amesisitiza waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanatekeleza amri ya kima cha chini cha mshahara na serikali itaendelea kufuatilia ili wafanyakazi walipwe kulingana na mapendekezo ya Bodi ya kima cha chini cha mshahara.