Seheme ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yakijiri katika hafla ya ufunguzi wa Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama iliyotolewa na Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Na Mary Gwera, Mahakama-Mwanza
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ameihimiza Mahakama nchini kujielekeza kufanya maboresho yenye kupunguza urasimu na kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri, hususani ya madai ili wananchi waweze kupata huduma za utoaji haki kwa gharama nafuu.
Akizungumza na Majaji na sehemu ya Watumishi wa Mahakama wakati akifungua Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 leo tarehe 12 Aprili, 2023 katika Hoteli ya Malaika jijini hapa, Mhe. Dkt. Mpango amesema kuwa, gharama kubwa za uendeshaji wa mashauri muda mwingine huongezeka kutokana na ucheleweshaji.
“Naupongeza Mhimili wa Mahakama kwa maboresho makubwa iliyofanya na inayoendelea kufanya, pamoja na maboresho hayo bado kuna maeneo mengine yanayopaswa kufanyiwa kazi, maeneo hayo ni pamoja na gharama kubwa za kuendesha mashauri ya madai, hivyo ni muhimu kuangalia namna ya kupunguza gharama hizo ili kuwapa unafuu wananchi,” amesema Makamu wa Rais.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Mpango amezungumzia suala la rushwa ambapo ameeleza kuwa, bado kuna baadhi ya malalamiko yanayotolewa na wananchi kuhusu uwepo wa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya Maafisa wa Mahakama, hivyo imeitaka Mahakama kufanyia kazi hisia za wananchi kuhusu suala hilo na kuziba mianya na viashiria vyote.
Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais amepongeza jitihada au maboresho ya Mahakama katika matumizi ya TEHAMA na kuhimiza haja ya kuongeza matumizi hayo kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa kada za chini ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani.
Aidha; Kiongozi huo wa Taifa ameitaka pia Mahakama kuendelea kusogeza huduma za Mahakama za Mwanzo ili kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi.
“Nafahamu kuna jitihada za uboreshaji miundombinu ya majengo ya Mahakama zimefanyika, lakini bado kuna uhitaji wa kusogeza zaidi huduma za Mahakama za Mwanzo karibu na wananchi kwakuwa idadi ya Mahakama hizo bado haitoshi kukidhi ongezeko la mashauri yanayofunguliwa na wananchi,” ameeleza Mhe. Dkt. Mpango.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa, kikao hicho kinalenga kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Mahakama pamoja na kutafuta namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili.
“Mkutano huu utatoa nafasi ya kutathmini kama huduma za Mahakama zimekidhi matarajio ya wananchi wa Tanzania kutokana na maboresho yaliyofanyika. Kikao hiki pia Kitatathmini namna Mahakama ilivyotimiza matarajio ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kuhusu maboresho ya utoaji haki ambayo ilizisukuma hadi kufikia makubaliano ya kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 91 zitumike katika maboresho kuanzia Februari 2022 hadi Desemba 2025,” amesema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu amewaelekeza Majaji, Mahakimu na Wamiliki wa Mradi wa Maboresho ya Mahakama, kutoishia kujitathmini kwa kuhesabu idadi ya mashauri yaliyokamilishwa, bali kutathmini utendaji wa haki unaozingatia vigezo vilivyotajwa katika Ibara ya 107A (2) ya Katiba (1977).
“Tunapofanya tathmini ya huduma zetu ni vyema kuzingatia takwa la kikatiba, yaani kuzingatia Sheria wakati wa kusikiliza na kutoa uamuzi; kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi; kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi, kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro; na kutenda haki bila kufungwa au kupita kiasi na masharti ya kiufundi,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Akizungumzia suala la rushwa, Jaji Mkuu amesema kwamba, bado Mahakama ina changamoto kadhaa ikiwemo tuhuma za rushwa. Ameongeza kwamba, matarajio ya wananchi ni kupata huduma bora zisizo na hisia au viashiria vya rushwa hivyo ameagiza watumishi na viongozi wote wa Mahakama katika Mkutano kufanya tathmini ya uhalisia, mianya, vipenyo, viashiria na perception ya rushwa.
Kuhusu utekelezaji wa mradi wa maboresho hadi kufikia Desemba 2022, Mhe. Prof. Juma amesema kwamba, mlundikano wa mashauri mahakama umepungua (backlog clearance) kutoka asilimia 11 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 6 mwezi Desemba, 2022, Kiwango cha kumaliza mashauri (case disposal rate) kiliongezeka kutoka asilimia 78 mwaka 2021 hadi kufikia 84 mwezi Desemba, 2022.
Katika kikao hicho cha siku tatu (3) Mada mbalimbali zitatolewa pamoja na kuwawezesha Maafisa hao wa Mahakama kufanya tathmini na kupendekeza maeneo ambayo huduma za utoaji haki zinatakiwa kubadilika ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora ya utoaji haki.