Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya kilimo katika eneo la utafiti kutoka Shilingi bilioni 11.5 hadi Shilingi bilioni 40.7 kwa mwaka wa fedha 2022/23, TARI-Dakawa kwa msimu huu wa kilimo, inatarajia kuzalisha tani 150 za mbegu za zao la mpunga kutoka tani 104 zilizozalishwa msimu uliopita.
Meneja TARI – Kituo cha Dakawa, Dkt. Jerome Mghase ameyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari – MAELEZO jinsi ongezeko la bajeti ya utafiti lilivyowasaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu za zao hilo.
Dkt. Mghase ameongeza kuwa, katika bajeti hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita imeiwezesha TARI-Dakawa fedha takriban Shilingi milioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa ghala la kuhifadhia mbegu ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 300 za mpunga,
“Tunaendelea kumshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia kwa kuwekeza fedha nyingi kwenye kilimo kwani mbali na bajeti kubwa ya utafiti, bado tumepata fedha zingine jumla ya Shilingi milioni 90 kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambazo zimewezesha kuongeza maeneo ya uzalishaji wa mbegu kutoka ekari 80 hadi ekari 120 ambazo zimeendelea kuongeza wigo wa uzalishaji mbegu wa zao hili”. Alisema Dkt. Mghase.
Vile vile Dkt. Mghase ameongeza kuwa, kutokana na mahitaji ya mbegu bora nchini kuongezeka mwaka hadi mwaka, taasisi hiyo imejipanga kupanua eneo la uzalishaji wa mbegu za zao hilo katika maeneo mengine hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya mahitaji hayo.
Akizungumza kuhusu mbegu bora zinavyowafikia wakulima, Mratibu Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano kutoka TARI-Dakawa, Fabiola Langa amesema ili kuhakikisha teknolojia bora za kilimo ambazo zimegunduliwa na taasisi zinawafikia wakulima na wadau wengine wa kilimo katika mnyororo mzima wa thamani, huwa wanaweka mashamba mfano hasa kwenye maeneo ya wakulima wanayolima ili waweze kufahamu aina gani ya mbegu inayolingana na mazingira yao.
“Mbali na teknolojia ya matumizi ya mbegu bora, tunapeleka tekonolojia mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo zikiwemo za kanuni za kilimo bora zitakazopelekea kuzalisha kwa tija, matumizi sahihi ya mbolea na viuatilfu pamoja teknolojia za kuongeza thamani kupitia zao hilo ikiwemo kutumia mchele kutengeneza unga na tambi.” Alisema Fabiola Langa.
Kwa upande wake Mkulima wa zao hilo, Nasibu Katoto amesema kuwa kilimo chake kimeboreshwa kutokana na maelekezo, mafunzo na mbegu bora kutoka katika taasisi hiyo, vile vile amewashukuru wataalam wa taasisi hiyo kwa kuwashirikisha wakulima kuelezea changamoto ya mbegu wanazozitumia ili waendelee na utafiti na kuleta mbegu bora.
“Kwa sasa ninapata faida kubwa, huko zamani uzalishaji ulikuwa kwenye gunia 10 mpaka 15 lakini kwa sasa uzalishaji wa chini ni gunia 30, hivyo uwepo wa kituo hiki na kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu kumesaidia wakulima wengi kupata mbegu bora na kwa urahisi”, alisema Katoto.