Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 lililojengwa katika kijiji cha Namalombe wilayani Masasi likiwa limekamilika
Meneja wa Ruwasa mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Damas wa kwanza kushoto na baadhi ya watumishi wa Ruwasa wakisubiri Mwenge wa Uhuru katika mradi wa maji Namalombe.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Namalombe wilayani Masasi wakisubiri kuupokea Mwenge wa Uhuru kijijini hapo.
Wakazi wa kijiji cha Namalombe wilayani Masasi wakifurahi Mwenge wa Uhuru ulipowasili katika kijiji hicho kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji uliotekelezwa na Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 500.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Masasi Juma Yahaya akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo.
Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cecil Mwambe akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namalombe mara baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji .
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,akizungumza na wananchi wa kijiji cha Namalombe na viongozi wa wilaya ya Masasi mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji.
Baadhi ya watumishi wa Ruwasa wakiongozwa na Meneja wa Ruwasa mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Damas wa nne kutoka kushoto waliosimama wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Namalombe.
Na Muhidin Amri,
Masasi
WAKAZI wa kijiji cha Namalembo kata ya Msikisi wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwajengea mradi wa maji uliomaliza mateso na kero ya maj ya muda mrefu.
Wakizungumza jana baada ya Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji Namalembo walisema, kabla ya mradi huo kujengwa sehemu kubwa ya maisha yao walitegemea kupata huduma ya maji katika Mto Mbangala uliopo kilomita 5 kutoka kwenye makazi yao.
Mohamed Ndelekaje alisema, hali hiyo ilisababisha kukosa muda wa kufanya shughuli za maendeleo kwa kuwa walitumia muda mwingi katika kutafuta maji, jambo lililochangia hata baadhi ya kaya kuwa maskini.
Alisema, mradi huo umewakomboa kwenye changamoto ya maji ambapo sasa watatumia muda wa wao kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Ndelekaje ameishukuru serikali kupitia Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambao unakwenda kumaliza kabisa changamoto ya maji na kuchochea maendeleo kuanzia ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.
Husna Mohamed alisema, kwa muda mrefu walitumia maji ya Mto Mbangala ambayo hayakuwa safi na salama kwani maji ya mto huo yanatumiwa na binadamu na wanyama pori.
Alisema, kujengwa na kukamilika kwa mradi huo kumewapunguzia adha kubwa ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwa ajili ya kutafuta tafutaji wa maji.
Meneja wa Ruwasa Wilayani Masasi Mhandisi Juma Yahaya alisema, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Ruwasa wilaya ya Masasi inatekeleza jumla ya miradi minane yenye jumla ya thamani ya Sh.bilioni 6.5 ambayo iko hatua mbalimbali za utekelezaji wake.
Alisema,miradi hiyo itakapokamilika itasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Masasi kutoka asilimia 73 hadi kufikia asilimia 80.
Akizungumzia ujenzi wa mradi wa Namalembo Eng. Juma alisema, Serikali imetenga kiasi cha Sh.milioni 517,610,167.42 kati ya fedha hizo wananchi wamechangia Sh.milioni 7 na Serikali kuu kupitia wizara ya maji imetoa Sh.milioni 510,610,167,.42.
Alisema,mradi wa maji Namalembo ulianza kujengwa mwezi Septemba 2022 kupitia kampuni ya Bison Engineering Co Ltd na lengo kubwa ni kuhudumia wananchi waishio katika kijiji cha hicho wapatao 4,094 kupata huduma ya maji karibu na makazi yao.
Alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa tenki la juu la mnara wa mita 9 la ujazo wa lita 100,000,ujenzi wa nyumba ya mashine(Pump House),uwekezaji wa mfumo wa umeme jua,ufungaji wa pump,ujenzi wa vituo wa vituo saba vya kuchotea maji.
Yahaya alitaja kazi nyingine zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa banio la kunyweshea mifugo,uwekezaji wa mtandao wa mabomba wenye jumla ya urefu wa mita 5,985 na ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake na umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanalipia huduma ya maji inayotolewa na kushirikiana na Serikali katika utunzaji wa miradi ya maji na miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa ili iwe endelevu na kusaidia katika suala zima la kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,amemwagiza Mkandarasi kampuni ya Bison Engineering Co Ltd ya Dar es slaam inayotekeleza mradi huo kukamilisha kazi kwa wakati.
Alisema, licha ya kujengwa kwa ubora na viwango vinavyotakiwa,lakini ni vyema mkandarasi aongeza kasi ya ujenzi wake ikiwezekana kabla ya muda wa mkataba, ili kutoa fursa kwa wananchi wa kijiji hicho wapate huduma ya maji safi na salama waliyokuwa wanaisubiri kwa muda mrefu.
Amewaagiza viongozi wa Ruwasa kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi huyo ili aweze kukamilisha kazi hiyo kama ilivyo katika makubaliano ya pande zote mbili wa Serikali na mkandarasi.
Amewataka viongozi wa serikali na mamlaka husika zilizopewa dhamana ya kusimamia mradi huo kutambua kuwa wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma yam aji kama ilivyokusudiwa.