Elimu ya utengenezaji wa sabuni ikiendelea kutolewa
Na Mwandishi wetu – Malunde 1 blog
Chuo cha Ufundi Stadi Kanda ya Magharibi Tabora kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wametoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vya wanawake kutoka vijiji vya Ikonda, Masengwa, Bubale na Ilobashi vilivyopo katika kata ya Masengwa wilaya ya Shinyanga.
Mafunzo hayo ya ujasiriamali yamefanyika kwa muda wa siku nne na kuhitimishwa leo Alhamis Aprili 6, 2023.
Wanawake zaidi ya 112 waliopo ndani ya kata ya Masengwa wamepewa elimu ya jinsi ya utengenezaji wa sabuni za miche, sabuni za kung’arishia vigae, dawa za kusafishia chooni, mafuta ya mgando pamoja na mbinu za ujasiriamali zitakazowawezesha wakazi wa kata hiyo kujiajiri na kujiinua kiuchumi.
Meneja wa masoko na ajira VETA Kanda ya Magharibi Tabora Nyongo Kihenge amesema mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea wananchi uwezo ili kujikwamua kiuchumi.
“Mara nyingi mamlaka ya mafunzo ya elimu na ufundi stadi huwa inatoa mafunzo kwa vikundi vya wajasiriamali ambao wako katika sekta isiyo rasmi ili kuweza kuongeza tija kwenye shughuli wanazozifanya au kuwapa ujuzi mpya utakaowawezesha kujiongezea kipato cha mtu mmoja mmoja , familia na jamii kwa ujumla”, amesema Nyongo Kihenge.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mkuu wa chuo cha ufundi stadi VETA Shinyanga Magu Mabelele ameeleza malengo ya mafunzo hayo kuwa ni pamoja na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja kwenye jamii na kuwasihi kutumia mafunzo hayo waliyopewa kujinufaisha kwa kuanzisha vikundi vya uzalishaji wa bidhaa walizofundishwa.
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo na kuwawezesha ikiwa na lengo la kuona matokeo chanya katika kata ya Masengwa,hivyo mafunzo haya ni mafunzo ambayo yameletwa kwenu kwa ajili ya kuwajengea uwezo na lengo kubwa ni kupunguza umaskini na kuongeza kipato kwenye kaya zetu, niwasihi ujuzi huu mlioupata mkautumie vyema”, amesema Magu Mabelele.
“Baada ya kupokea mafunzo haya mnaweza kuanzisha vikundi vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali vitakavyojihusisha na utengenezaji wa sabuni na bidhaa mlizofundishwa, ili kuweza kunufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri zetu”, ameongeza Magu Mabele.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kata ya Masengwa Atupokile Maseta amewasihi wanawake hao kuzingatia uhitaji wa masoko ili kunufaika na walichojifunza kupitia mafunzo hayo.
“Kwanza niwapongeze kwa kushiriki mafunzo haya lakini ili kunufaika na hiki tulichojifunza hapa twendeni tukazingatie uhitaji wa masoko ya maeneo yetu tuliopo ili bidhaa tutakazo tengeneza zikalete tija kwetu na jamii kwa ujumla”, amesema Atupokile Maseta.
Mkuu wa chuo cha ufundi stadi VETA Shinyanga Magu Mabele akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo.
Elimu ya utengenezaji wa sabuni ikiendelea kutolewa
Elimu ya utengenezaji wa sabuni ikiendelea kutolewa
Sabuni iliyotengenezwa na washiriki wa mafunzo hayo
Sabuni iliyotengenezwa na washiriki wa mafunzo hayo
Mkuu wa chuo cha ufundi stadi VETA Shinyanga Magu Mabelele akitoa cheti cha kuhitimu mafunzo hayo kwa mmoja wa wakazi wa kata ya Masengwa.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Masengwa wakiwa kwenye mafunzo hayo.