NA FARIDA MANGUBE MOROGORO.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuiwakilisha Serikali kwa ufanisi katika Mashauri yote ya Madai na Usuluhishi, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Februari, 2023 Ofisi iliendesha jumla ya mashauri 6,263 ikiwemo mashauri 6112 ya madai na mashauri 151 ya usuluhishi.
Akifungua kikao cha pili cha baraza la pili la wafanyakazi wa ofisi ya wakili mkuu wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023Wakili mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Nalija Luhende amesema ofisi hiyo kufanikisha kumaliza mashauri/migogoro mbalimbali kwa njia ya majadiliano, usuluhishi na maridhiano nje ya Mahakama.
“Katika mwaka wa fedha 2022/23, Ofisi imeweza kumaliza migogoro mbalimbali kwa njia ya majadiliano, migogoro hiyo inajumuisha, mashauri ikiwamo, shauri la Usuluhishi lililofunguliwa dhidi ya Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Usuluhishi ya jijini London.” Alisema Dkt. Luhende.
“ Katika shauri hilo, Serikali ilikuwa inadaiwa takribani Dola za Marekani Billioni 3 sawa na fedha za Kitanzania Trilion 7 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikishirikiana na Timu maalum ya Majadiliano ya Serikali iliweza kumaliza shauri hili kwa majadiliano nje ya usuluhishi.” Aliongeza
Aidha amesema Ofisi iliweza kumaliza kwa majadiliano shauri la Usuluhishi lililofunguliwa dhidi ya Serikali ya Tanzania kwenye Baraza la kimataifa la usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC) ambalo wadai walikuwa wanadai kiasi cha dola za Marekani Milioni 72 sawa na Billion 170 za Kitanzania.
Kwa upande wake Naibu wakili mkuu wa Serikali Bi. Sarah Duncan Mwaipopo amsema madhumuni ya mkutano huu ni kuwawezesha wafanyakazi kupitia Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya Bajeti ya OWMS.
Amesema katika Mwaka huo wa fedha OWMS imejiwekea Malengo nane tofauti na Mwaka wa Fedha 2022/23 uliokuwa na Malengo sita ambapo malengo mawili yaliyoongezeka ni mtambuka kwa kuwa Serikali imeelekeza Wizara, Taasisi za Serikali na Serikali za Mitaa kutenga na kuongeza kwenye Bajeti Mazingira na Lishe.