Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia tawi la JKCI uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia Taifa Dkt. Samuel Rweyemamu akizungumza na wanachama wa chama hicho tawi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Katibu wa chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia tawi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. George Longopa akizungumza na wajumbe wa mkutano huo wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Wanachama wa chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia tawi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa umoja, ushirikiano na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuleta ufanisi na tija kazini .
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa JKCI.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kukiwa na ushirikiano wa vyama vya wafanyakazi, wafanyakazi na uongozi kunasababisha watu kufanya kazi kwa kujituma na kutoa huduma bora kwa wagonjwa lakini kama hakuna ushirikiano atakayeumia ni mgonjwa.
“Dira ya Taasisi yetu ni kuwa kiwango cha juu kimataifa kwa usimamizi, utafiti na mafunzo ya moyo haya yote yatawezekana kama tutafanya kazi kwa pamoja na kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanapatikana, kusikiliza changamoto za wafanyakazi na kuzifanyia kazi”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema viongozi wa chama hicho bado wanakazi kubwa ya kuwakusanya pamoja madaktari na wafamasia ili waweze kutetea maslahi yao na kushirikiana katika taaluma zao.
“Angalieni namna ya kufanya uwekezaji mkubwa ili chama kipate fedha zaidi na kuweza kujiendesha zaidi kuliko kutegemea fedha za michango ya wanachama”, alishauri Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Dkt. Samuel Rweyemamu aliushukuru uongozi wa Taasisi hiyo kwa kukiwezesha chama hicho kufanya kazi zao bila tatizo lolote lile.
Dkt. Rweyemamu alisema lengo la kuanzishwa kwa chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia ni kutetea maslahi ya wanachama hivyo basi ni muhimu wanachama hao wakaungana kwa pamoja na kutetea haki zao za msingi.
“Madaktari na Wafamasia wanakutana na changamoto mbalimbali za kazi hivyo basi kama tutaungana kwa pamoja na kuweza kutatua changamoto hizi tunaweza kufika mbali zaidi na kufanya kazi zetu bila ya kuwa na manung’uniko”, alisema Dkt. Rweyemamu.
Naye katibu wa chama hicho Tawi la JKCI aliyemaliza muda wake Dkt. George Longopa alisema ni muhimu kwa madaktari na wafamasia wakaona umuhimu wa kujiunga na chama hicho ili waweze kufanya maamuzi ya pamoja.
“Chama hiki ni muhimu kwani kinawakusanya watu wa kada moja ambao wanakutana na kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata fursa za mafunzo na kutatua changamoto zinazowakabili”,alisema Dkt. Longopa.
Katika mkutano huo pia ulifanyika uchaguzi wa viongozi watakaoongoza chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia tawi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha miaka miwili ambapo Dkt. Tryphone Kagaruki alichaguliwa kuwa mwenyekiti, Mfamasia Hadija Madende mwenyekiti wanawake, Dkt. Khairoon Mohamed mwenyekiti vijana, Mfamasia Yusuph Mwakatobe katibu na Dkt. Nakigunda Kiroga katibu wanawake.
Wajumbe waliochaguliwa ni Dkt. George Longopa, Mfamasia Miraji Dhahir , Dkt. Honoratha Maucky na Mfamasia Ndenasha Kimario.