Baadhi ya wanafunzi wa hule ya Sekondari Mbawala Halmashauri ya wilaya Mtwara wakiwa katika picha ya pamoja na Mhandisi Aloyce Milyangula wa kwanza mstari wa nyuma kutoka ofisi ya meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu.
Mwanafunzi wa kidato cha pili Fatma Hamis akichota maji katika kituo kinachotoa huduma ya maji kilichojengwa shuleni hapo.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Mbawala Halmashauri ya wilaya Mtwara wakifurahi huduma ya maji baada ya Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa)kufikisha huduma ya maji katika shule hiyo.
Muhidin Amri,
Mtwara
KERO kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Mbawala Halmashauri ya wilaya Mtwara mkoani Mtwara kutembea zaidi ya kilomita mbili kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya kila siku shuleni hapo imebaki kuwa Historia.
Kero hiyo imemalizika baada ya wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Mtwara kufikisha mtandao wa maji ya bomba katika shule hiyo.
Wanafunzi wa shule walisema,hapo awali walipata wakati mgumu katika masomo yao kwani kabla ya kuingia madarasani kuanza masomo walilazimika kwanza kwenda kutafuta maji yanayopatikana kwenye mabonde ama kuchimba mashimo kwa mikono hali iliyosababisha kukosa baadhi ya vipindi.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo Fatma Hamis alieleza kuwa,kukosekana kwa maji safi na salama kulisababisha mazingira ya shule kuwa machafu na wanafunzi kwenda shule wakiwa wachafu.
Aidha alisema,baadhi ya wanafunzi wameamua kuacha masomo ili kuepuka usumbufu wa kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya shule hasa usafi wa vyoo na mazingira kwa ujumla.
Fatuma,ameishukuru serikali kupitia Ruwasa kutekeleza mradi huo ambao umewezesha kupata muda mwingi wa kujisomea na kuepukana na magonjwa mbalimbali kama kichocho na magonjwa mengine yanayotokana na uchafu.
“miaka yote miwili tulisoma kwa shida sana kutokana na ukosefu wa maji safi na salama,tulilazimika kwenda kuchota maji yaliyojaa matope kwenye visima vya asili na mbaya zaidi maji hayo yalikuwa machafu na yasiofaa kwa matumizi ya binadamu kwa ajili ya matumizi ya kila siku”alisema.
Mwalimu wa zamu Bakari Rajabu alisema,tangu shule hiyo ilipoanzishwa miaka kadhaa changamoto kubwa ilikuwa ukosefu wa huduma ya maji ambapo wanafunzi walilazimika kutembea kilomita mbili hadi tatu kwenda kutafuta maji ili yatumike kwa shughuli za usafi na shughuli nyingine muhimu.
Alisema,hali hiyo ilisababisha mahudhurio madogo kwa wanafunzi ambao wakati mwingine kabla ya kuingia madarasani walilazimika kwenda kutafuta maji yanayopatikana mbali na eneo la shule, hivyo kusababisha wanafunzi kuchelewa vipindi vya masomo na hata kuathiri kazi ya ufundishaji.
Mwalimu Rajabu alisema baada ya kupata mradi wa maji safi na salama,mahudhurio ya wanafunzi yameongezeka na kuishukuru serikali ya awamu ya sita kujenga mradi huo ambao umesaidia sana kuinua taaluma na kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi.
Kwa upande wake Mhandisi wa maji kutoka ofisi ya Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mtwara Aloyce Milyangula alisema,Ruwasa imelazimika kujenga mradi huo ili kutatua tatizo la upatikanaji wa huduma iliyokuwepo kwa muda mrefu na kusababisha kutokea kwa magonjwa ya milipuko ya mara kwa mara.
Alisema,shida ya maji ilipelekea hata kusua sua kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa kuwa wananchi walilazimika kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku badala ya kufanya kazi za kujiletea kipato katika familia zao.
Alisema,baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo wananchi wamehamasika kwa kuvuta maji majumbani ambapo hadi tayari zaidi ya kaya kumi zimeingiza maji kwenye nyumba zao na wengine wakiendelea kuleta maombi ili kupata huduma ya kuunganishiwa maji majumbani.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mtwara Anastanzia Wambura, amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira na vyanzo vya maji ili miradi inayojengwa iwe endelevu kwa faida ya kizazi cha sasa na kinachokuja.
Alisema,serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi ya maji,hivyo ni wajibu kwa kila mwananchi kuwa mlinzi na kutumia maji hayo katika shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kuanzisha kilimo cha bustani.
Wambura alisema,miaka ya nyuma hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya na mkoa wa Mtwara ilikuwa changamoto na mateso makubwa,lakini tangu serikali ya awamu ya sita iingie madarakani hali hiyo imeanza kupungua na wananchi wameanza kufaidi matunda ya serikali yao.