Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na watalaam wa Afya mkoa wa Kagera pamoja na wadau mbalimbali inaendelea na jitihada za uelimishaji jamii juu ya ugonjwa wa Marburg, jumla ya wanafunzi 2723 katika shule 6 za msingi kata ya Katoma Wilayani Bukoba Mkoani Kagera wamefikiwa na elimu hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Dkt.Tumaini Haonga ikiwa ni katika mwendelezo wa uelimishaji , Beauty Mwambebule amesema lengo la serikali ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi ili wawe mabalozi wa utoaji wa elimu jinsi ugonjwa wa Marburg unavyoenezwa na jinsi ya kujikinga.
“Lengo ni kuweka nguvu ya pamoja katika kuhakikisha wanafunzi wengi wanapata elimu hii jinsi ya kujikinga na Ugonjwa wa Marburg kwani tunaamini hawa wanafunzi watakuwa mabalozi katika kuelimisha jamii imenipa faraja kuwa ujumbe huu umefika kwa wakati sahihi, kwa watu sahihi kwani ukielimisha wanafunzi umeelimisha taifa zima”amesema.
Nao baadhi ya wanafunzi waliofikiwa na elimu hiyo akiwemo Elius Erick kutoka shule ya Msingi Kilaini amesema ujumbe aliopewa ataufikisha nyumbani na sehemu nyingine ya jamii.
“Kupitia elimu hii nimenufaika sana na huu ujumbe nitaufikisha nyumbani kuanzia sasa nimeelewa kama mtu akitapika anaweza kuambikiza watu wengine wakigusa matapishi hivyo nitakuwa makini kuchukua tahadhari “amesema.
Naye Azadi Audax mwanafunzi darasa la Saba amesema kupitia ujumbe huo kuanzia sasa amejua kuwa ugonjwa wa Marburg unaweza kuambukizwa kwa kugusa jasho hivyo atakuwa makini kuchukua tahadhari kuchukua tahadhari.
“Mambo mengi nimenufaika na ujumbe huu ambao mmetoa hivyo kuanzia sasa najua jasho pamoja na kushika kinyesi naweza kupata ugonjwa wa Marburg”amesema.
Jeneroza Vedasto ni mwanafunzi kutoka shule ya Msingi Rwakagondo amesema kuanzia sasa amejua dalili za ugonjwa wa Marburg ikiwa ni pamoja na kutapika , kuharisha, na homa kali.
“Nimeelewa jinsi ya kuepuka ugonjwa wa Marburg, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni ya maji na dalili nazitambua kuanzia leo mfano kutapika ,kutokwa na damu”amesisitiza.
Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa katika zoezi hilo la uelimishaji ikiwa ni pamoja na swali la mwalimu Sophia John kutoka shule ya Msingi kilaini aliyehoji tahadhari gani achukue pindi anapogusa madaftari ya wanafunzi pindi anaposahihisha, Mwanafunzi Yusufu Mganizi kutoka shule ya Msingi Rwakagondo aliyehoji iwapo mtu mwenye maambukizi amekula chakula kikabaki je, kinaweza kuambukiza wengine, amabapo mwanafunzi Magreth Ndila alihoji je,kinyesi cha mtoto mwenye maambukizi kinaweza kuambukiza wengine .
Mwanafunzi Elin Gidius amehoji je, jasho la mtu akiwa anapika likidondokea kwenye uji wa moto linaweza kuambukiza Marburg huku mwanafunzi Johson Kerazi akiuliza ugonjwa wa Marburg unaweza kuambukiza Wanyama wa kufugwa.
Baadhi ya shule zilizopatiwa elimu ya Marburg ni pamoja na shule ya Msingi Kilaini wanafunzi 519, Shule ya Msingi Rwakagondo(416), shule ya Msingi Katoma “A”(461),Shule ya Msingi Katoma “B”(376), shule ya Sekondari Katoma Wanafunzi 574 na shule ya Kalwoshi wanafunzi 377 jumla ikiwa ni wanafunzi 2723 wamenufaika na elimu ya Marburg.