Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KAMATI ya Futari Mkoani Pwani ,imetoa vyakula kwa ajili ya iftari katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadan kwa Taasisi 20 pamoja na Magereza ya Mkuza.
Akigawa vyakula hivyo , Sheikh Mkuu Mkoani Pwani ,Hamis Mtupa ambae pia ni Mlezi wa kamati hiyo ,alieleza ni muendelezo wa ugawaji wa iftari tangu izinduliwe Machi 18 mwaka huu.
Alieleza kamati hiyo imepokea maombi mbalimbali,hivyo wanaendelea kuwaomba wadau kuchangia na kupokea michango ili kuwafikia wahitaji katika mwezi huu.
“Kila kitu hatua ,tunapendelewa kukusanya michango,tunaamini tutafikia walio wengi kwa kuanzia na hizi Taasisi ikiwemo shule na Magereza,Jambo hili tangu lianzishwe limekuwa msaada ,tunajipambanua ili miaka ijayo tuwe msaada zaidi, Hata Mufti Abubakari Zuberi amekuwa akishuhudia hili amefarijika kwani inasaidia kutoa futari ,.”
Aidha Mtupa , aliwaasa Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kazi kubwa anayoifanya kukuza uchumi na kuinua maendeleo ya nchi.
Vilevile alieleza, Ramadan ni chuo Cha maadili, wakati huu watu wanaishi kwa maadili hivyo waendeleze yote mema kwa wakati wote.
Mtupa aliiasa jamii kuacha mambo ya mmomonyoko wa maadili , watu washirikiane bila kujali udini ,ukanda ama itikadi zao na waendelee kuliombea Taifa ili liendelee kuwa kisiwa cha amani.
Awali Mwenyekiti wa kamati ya iftari Mkoani Pwani, Omari Khatibu alieleza, kamati imetoa vyakula , mchele,mafuta ya kula,tende,tambi , sukari,unga wa ngano kwa Taasisi 20 ikiwemo shule mbalimbali na Magereza ya Mkuza.
Alisema ,Jumla ya watakaopata sadaka hiyo ya iftari ni 2,098 kutoka kwenye Taasisi hizo.
Muhammad Tundia alisema kamati hiyo ilianza mwaka 2018 ikiwa na kazi kubwa ya kupokea michango ya jamii ili kupata iftari kwa waja wa Allah kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadan.
Alieleza,kamati imekuwa ikitoa kutokana na kinachopatikana na wanaamini uchangiaji utakuwa zaidi ya Sasa.
Mwanafunzi kutoka Ruvu Jamila Humoud na Mwanafunzi wa Mwanalugali Mshauri Ally wamemshukuru kwa msaada wa futari walioupata na kusema mungu awaongezee waliojaliwa kuchangia.