Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
WAZIRI wa Ulinzi na JKT , Innocent Bashungwa (mb) ,ameeleza katika kutekeleza dira ya Serikali ya awamu ya sita kuinua sekta ya uwekezaji atahakikisha wizara hiyo inashirikiana na vyombo vingine vya jeshi kujenga sekta ya viwanda na ulinzi.
Akikabidhi magari matatu ya zima moto yaliyotengenezwa na shirika la Nyumbu kwa wizara ya mambo ya ndani ya nchi,huko Nyumbu,Kibaha Mkoani Pwani, Bashungwa alieleza, hatua hiyo ni kielelezo cha uthubutu wa majeshi hayo kutengeneza kitu kikubwa cha kuheshimisha nchi na kusaidia kutimiza wajibu wao.
Alisema, hayo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona Wizara inashirikiana na vyombo vingine ambapo katika muelekeo huo,wanayo mashirika mawili ya ulinzi Shirika la TATC Nyumbu na Mzinga ambayo yaliasisiwa na Hayat Mwl. Julius Nyerere .
“Kwasasa Mzinga kwa muelekeo mpya wa Shirika na TACT yapo mstari wa mbele kuhakikisha dira hiyo inatimizwa “
Vilevile ,Bashungwa aliipongeza TACT Nyumbu kwa kushirikiana na Jeshi la zimamoto kutengeneza magari hayo yenye viwango vya kimataifa.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa nyenzo,mafunzo,vitendea kazi na ajira.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini alisema watahakikisha wanayatunza magari hayo,na kusaidia katika utendaji kazi.
Nae makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya ulinzi na usalama, Vicent Mbogo alilitaka Shirika la Nyumbu kujitangaza na kuainisha changamoto zao ziweze kupatiwa ufumbuzi ili kujiendesha kwa ufanisi.
Kamanda wa kikosi cha jeshi na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Nyumbu,Brigedia Jenerali, Hashim Komba alieleza kwamba, mradi wa gari la zimamoto Ulianza Mwaka 1986 hadi 1991 kwa kufanikiwa kuunda magari ya zimamoto aina
tatu; Municipal Fire Tender kwa ajili ya maeneo ya miji, Rapid
Intervention Vehicle kwa ajili ya viwanja vya ndege na Fire Crash
Tender kwa ajili ya viwanja vikubwa vya ndege na vituo vya mafuta.
Hashim alisema, kuhusu mkataba wa kukarabati Magari mabovu ya Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji, Shirika lilisaini makubaliano na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kukarabati magari
mabovu idadi kumi na mbili ya kiwango cha Manispaa, Mkataba mwingine Shirika lilisaini makubaliano na
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuunda magari mapya
idadi matatu (3) ya kiwango cha Manispaa kwa kutumia Rolling
Chassis ya Scania kulingana na hitajio la mteja wao.