Kaimu Rasi wa Ndaki ya Uchumi Kilimo na stadi za Biashara Dkt. Zena Mpenda akifungua warsha ya Wadau wa Mradi wa TRADE HUB kujadili matokeo ya utafiti.
Na Amina Hezron,Morogoro
WADAU wa zao la Soya kahawa miwa na nyama pori wametakiwa kushiriki
kikamilifu kwenye kutoa mapendekezo na
maoni yao kwenye Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendeleo na Mazingira (TRADE
Hub) ili matokeo yatakayopatikana yaweze kuinua tija ya mazao hayo nchini.
Hayo yameelezwa na Kaimu Rasi wa Ndaki ya Uchumi Kilimo na stadi za
Biashara Dkt. Zena Mpendu aliyemuwakilisha Rasi wa Ndaki hiyo Dkt Damas Philip
katika warsha iliyoandaliwa na mradi huo
ili kuwasilisha matokeo ya awali ya utafiti wao kwa wadau ili kupata maoni
yao juu ya namna bora ya kufanya
biashara ya haki na endelevu.
Amewataka wadau hao kuzingatia kuwa tasnia hizo zinagusa kwa namna moja ama
nyingine maisha na maendeleo ya wadau mbalimbali pamoja na uchumi na maendeleo
ya nchi kwa ujumla hivyo watumie fursa hiyo kwa makini kutoa maoni yao ya namna
bora ya kuboresha biashara katika tasnia
hizo zote za Nyama pori na Mazao ya kilimo.
“Ni vizuri tunaposikiliza hizi mada zinazotolewa tuangalie inaelezea kweli
ile hali halisi kwenye maeneo yetu ili tuweze kuboresha yale ambayo tumeyaona
lakini pia tuweze sasa kuangalia mapendekezo yanayotoka tuone hayo mapendekezo
yatafanyika yanawezekana ili tukitoka hapa tuwe na mapendekezo ambayo ni bora
zaidi”, alisema Dkt. Zena.
Dkt. Zena ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikiboresha mara kwa mara Sheria,
taratibu na Kanuni kuhakikisha kwamba biashara hizo hazisababishi ongezeko la
uharibifu wa mazingira na upotevu wa baionuai hivyo ni muhimu kama wadau wa
biashara kuhakikisha wanaingia kwenye mikataba ya kijani kwenye biashaa zao ili
kuwe na biashara endelevu kwaajili ya watu na ulimwengu pia.
Akieleza malengo ya warsha hiyo Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA Prof.
Japhet Kashaigili amesema kuwa ni kuwasilisha kwa wadau matokeo ya tafiti
kadhaa ambazo mradi huo umeyapata ili wapate nafasi ya kuyajua, kuyajadili na
kutoa mapendekezo ili kuona ni namna gani yanaweza kuchangia kwenye maendeleo
ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Lengo lingine la pili la warsha yetu hii na mradi ni kutengeneza mpango au
njia itakayotupeleka nchi mahali fulani kuptia ufanyaji wa biashara yenye haki
na endelevu nchini Tanzania lakini pia bidhaa zetu ziweze kuhimili ushindani
kwenye masoko ya kimataifa na kukuza uchumi”, alifafanua Prof. Kashaigili.
Aidha amesema dhumuni kubwa linalobeba mradi huo ni kuhakikisha biashara ya
mazao na nyama pori inakuwa ni injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi,Kuondoa
umasikini na kama mbinu ya kutekeeleza maendeleo endelevu kama ilivyosisitizwa
kwenye Mpango wa maendeleo endelevu bila kuchangia uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa mradi huo Prof. Reuben Kadigi amesema warsha hiyo
ya wadau ni muhimu sana katika kupata maoni na mapendekezo ambayo yatawasaidia
watafiti kuweza kutengeneza andiko la sera ambalo litawasilishwa Serikalini ili
kusaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Kila mchango wa mdau unaotolewa andika mahali kila ushauri andika ili
mwisho wa siku tupate kitu kizuri kifupi cha kuwasilisha serikalini baada ya
kufanya uchambuzi wa kina kulingana na matokeo tuliyoyapata maana mwisho wa
siku hatuwezi kupeleka kwa watunga sera kitu kinacholeweka nawaweze kukifanyia
kazi kwa ustawi wa biashara nchini”, alieleza Prof. Kadigi.
Kwa upande wake Dkt. Charles Malaki aliyemuwakilisha Kaimu Rasi wa Ndaki
hiyo amewashukuru wadau waliojitokeza katika warsha hiyo na amewataka kutoa
maoni na mapendekezo ya kuboresha matokeo ya tafiti hizo ili kuisaidia Serikali
baadae kupata sera bora zitakazosaidia kuwa na uendelevu katika biashara ambayo
inajali Mazingira,Nyama pori pamoja na watu.
Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendelo na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa
miaka mitano unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa
kushirikiana na washirika wengine kutoka katika nchi kumi na tano za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil kuanzia
Februari 2019 hadi Machi 2024.