Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Ziara za Ramadhani ni fursa muhimu ya kurudisha enzi za kusaidiana katika kuzikabili changamoto mbali mbali za maisha ya watu hapa Nchini.
Mheshimiwa Othman, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, ameyasema hayo leo Machi 28, huko Mwera Pongwe, Mkoa wa Kati Kichama, kisiwani Unguja, katika muendelezo wa ziara zake za kuwatembelea na kuwakagua wagonjwa na wazee mbali mbali kwa lengo la kuwafariji.
Amesema kuwa mwenendo huo ambao ni utamaduni uliorithiwa tangu zamani na wazee hata waliotangulia, unalenga kulinda na kurejesha zile enzi ambazo jamii iliishi kwa kusaidiana katika kuzikabili na kuzitatua changamoto mbali mbali zikiwemo za hali ngumu ya maisha.
Mheshimiwa Othman amebainisha kuwa ziara hizo, pamoja na mambo mengine, zinalenga kujenga ukaribu kwa wananchi sambamba na kubaini changamoto mbali mbali zinazowakabili, ambapo huo ni wajibu wa dhati wa kila kiongozi wa kweli.
Aidha Mheshimiwa Othman amekiri kuwepo hali ngumu ya maisha pamoja na wimbi la migogoro ya ardhi ambayo imeota mizizi sasa hapa Zanzibar na Tanzania yote.
Ameeleza kwa kusema ni kweli ipo migogoro mingi ya ardhi hapa Nchini ambapo miongoni mwa sababu zake ni kwamba sasa raslimali hiyo imepanda thamani sambamba na ongezeko kubwa la watu.
Mhehishimiwa Othman ametoa ufafanuzi huo kufuatia salamu zilizowasilishwa mbele yake, kwa niaba ya wananchi, na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kati Unguja Kichama, Bw. Vuai Abdulkadir Makame, ambaye ameeleza juu ya hali ngumu ya maisha inayokwenda sambamba na kutokutendewa haki katika migogoro ya ardhi Nchini kote, na kwa kuzingatia matumaini ya watu kwa Viongozi wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hapa Visiwani.
Akiendelea kutolea ufafanuzi hoja za Kiongozi huyo, Mheshimiwa Othman ambaye ametolea mifano changamoto ya ardhi kuzidi kuwa mali katika Visiwa vya Unguja na Pemba, ametaja uwepo wa zaidi ya Hoteli 600 sambamba na ongezeko kubwa la wageni kutoka nje ya Zanzibar, wanaomiminika hapa kwa lengo la biashara au kujitafutia maisha.
‘Haya yanatokana pia na matatizo ya muda mrefu yakiwemo ya udhaifu au ukosefu wa mfumo bora wa kusimamia raslimali hiyo, licha ya baadhi ya hatua zilizoanza kuchukuliwa baada ya mashauriano, mathalan kwa kiasi fulani kuundwa kwa hizi kamati na mahakama maalum za usimamizi na utatuzi wa migogoro ya ardhi”, amefahamisha Mheshimiwa Othman.
Akiagana na Viongozi pamoja na baadhi ya Wananchi wa Mkoa huo, katika ziara yake hiyo, Mheshimiwa Othman amekaririwa akisema, “kubwa la msingi nawatakieni ‘Ramadhan Kareem’ na kumuomba Mungu Akubali Funga zetu, tuzidishe mshikamano ili iwe sababu ya kuendeleza Maridhiano yetu, ndani ya Visiwa vyetu na Tanzania kwa ujumla”.
Ziara hiyo iliyoanzia katika maeneo ya Kumbini na Kajengwa, Jambiani, Uroa, Chwaka na Kiboje katika Majimbo ya Makunduchi, Paje, Chwaka, Tunguu na Uzini yote ya Mkoa wa Kusini Unguja, imewahusisha baadhi ya Masheha wa Shehia pamoja na Viongozi mbali mbali wa ACT-Wazalendo, akiwemo Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Bw. Salim Bimani.