Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Alex Sonna-DODOMA
TUME ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imetaja mafanikio kumi (10) iliyopata katika kipindi cha awamu ya sita ikiwemo upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo kupitia Vyama vya Ushirika.
Mafanikio hayo yametajwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.
Dk. Ndiege amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Sekta ya Ushirika imepata mafanikio katika maeneo mbalimbali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Vyama vya Ushirika kutumia mifumo rasmi ya masoko ya mazao ya wakulima.
Mrajis anasema wakulima wameendelea kukusanya na kuuza mazao yao kupitia mfumo rasmi wa uendeshaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika.
Amesema hadi kufikia Januari 31 2023, zaidi ya tani milioni 1.8 zenye thamani ya Sh trilioni 1.7 za mazao ya Tumbaku, Korosho, Pamba, Kahawa, Ufuta, Kakao, Konge, Chai, Mbaazi, Soya, Zabibu, Miwa na Maharage zilikusanywa na kuuzwa kupitia Vyama vya Ushirika.
Amesema makusanyo ya mazao hayo yameongezeka kwa asilimia 67.30 kutoka tani 597,298.58 zilizokusanywa msimu wa 2021/22 hadi tani zaidi ya tani milioni 1.8 zilizokusanywa msimu wa 2022/23.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Abdulmajid Nsekela
Thamani ya mazao yaongezeka
Thamani ya mauzo ya wakulima yaliyouzwa kupitia Vyama vya Ushirika imeongezeka kwa asilimia 11.30 kutoka Shilingi 1,552,635,769,446 katika msimu wa 2021/22 hadi Shilingi 1,752,128,795,530 katika msimu wa 2022/23.
Upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo kupitia Vyama vya Ushirika
Dk.Ndiege amesema Pembejeo za Kilimo zenye thamani ya Shilingi 449,922,623,196 zilinunuliwa na kusambazwa kupitia Vyama vya Ushirika katika Msimu wa mwaka 2022/2023: Mbolea (mifuko 1,266,435) – Shilingi 227,983,187,800/; Viuatilifu (madawa) – Shilingi 138,598,132,500/; Vifungashio – Shilingi 53,163,612,896/; Mbegu – Shilingi 30,096,453,500/; na Miche – Shilingi 81,236,500/
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC Dkt. Benson Ndieg
Upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kuhudumia wanaushirika na wakulima kupitia Vyama vya Ushirika
Mtendaji huyo amesema Tume kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika pamoja na taasisi za kifedha, imeendelea kuratibu na kusimamia upatikanaji wa mikopo mbalimbali kupitia ushirika kwa ajili ya kuwahudumia wanaushirika na wakulima kwa ujumla.
“Mikopo hiyo imetolewa na taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya TADB PLC, CRDB PLC na NMB PLC kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo za kilimo, ujenzi wa ghala, ukusanyaji na uchakataji wa mazao na ujenzi wa mabani ya kukaushia tumbaku,”amesema Mtendaji huyo.
Amesema hadi kufikia Januari, 2023, jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi 77,582,588,029 pamoja na Dola za Marekani (USD) 75,393,670 ilitolewa na taasisi za kifedha.
Kukuza matumizi ya TEHAMA katika Vyama vya Ushirika
Dkt. Ndiege amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanzisha Mfumo wa TEHEMA wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) ambapo hadi kufikia mwezi Februari 2023, Tume imefanikiwa kusambaza na kutoa mafunzo kuhusu MUVU katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri.
“Wanufaika wa mafunzo hayo walikuwa 598 wakiwemo Maafisa TEHAMA 30, Warajis wasaidizi wa mikoa 26, Watendaji wa Bodi za Mazao 74, Maafisa Ushirika 392 na Mameneja na wenyeviti wa Bodi za vyama vikuu 76,”amesema
Aidha, mafunzo katika ngazi ya Vyama vya Msingi yametolewa kwa mikoa ya Dar es salaam, Simiyu, Iringa na Halmashauri ya Dodoma Jiji, Busekelo, Kyela, na Rungwe, ambapo Mameneja 1,790 na Wahasibu 102 walipata mafunzo. Matumizi ya MUVU yameanza ambapo jumla ya vyama 3,867 vimeishasajiliwa na kuhuisha taarifa.
Wanachama wa Ushirika waongezeka kufikia 8,358,326
Mrajis amesema Tume imeendelea kufanya uhamasishaji kwa lengo la kuongeza idadi ya wanachama wa vyama vya ushirika na kuimarisha shughuli za vyama.
Matokeo ya uhamasishaji huo ni kuongezeka kwa wanachama kutoka 6,965,272 mwaka 2021 hadi kufikia wanachama 8,358,326 Mwaka 2023 ambao ni sawa na asilimia 20 ya ongezeko la wanachama kwenye Vyama vya Ushirika.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili, uhamasishaji ulifanywa kwenye Skimu ya umwagiliaji ya Zabibu ya Lubala kwa lengo la kufufua Shamba la Chinangali lililopo chini ya uendeshaji wa CHABUMA AMCOS Ltd.
“Uhamasishaji wa Wanachama 4,468 wa AMCOS 7 wilayani Bahi wanaojishughulisha na kilimo cha mpunga kufanya shughuli zao kupitia Mfumo waUshirika Uhamasishaji kuhusu uanzishwaji wa Viwanda vidogo vya kuchakata zao la zabibu kuongezea thamani,”amesema Dkt. Ndiege.
Amesema TCDC imefanya Uhamasishaji kwa vikundi 76 vyenye jumla ya wakulima 3,177 vinavyojishughulisha na mazao ya bustani yaani Mbogamboga, Maua, Matunda na Viungo ili kuanzisha Vyama vya Ushirika vya mazao ya bustani katika mikoa ya Arusha, Njombe na Mbeya.
Ajira 146,545 katika Vyama Vya Ushirika
Vyama vya ushirika nchini katika kutekeleza shughuli zake hadi kufikia Machi 2023 vimeajiri Watanzania 146,545. Waliojiriwa kwa mkataba ni 38,209 na walioajiriwa katika ajira za msimu ni 108,346.
Mafunzo kwa Maafisa Ushirika na Watendaji wa Vyama
Dkt. Ndiege amesema Tume katika kuimarisha utendaji kazi hususan ukaguzi wa mara kwa mara na usimamizi wa vyama vya ushirika, imetoa mafunzo kwa Maafisa Ushirika 176 kutoka Mikoa 13 ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Njombe, Iringa, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Simiyu na Geita.
Aidha, Tume kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Shirika la Ukaguzi wa vyama vya Ushirika (COASCO), Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT); iliandaa Mpango wa mafunzo kwa watendaji wa vyama ambapo katika kipindi cha miaka miwili, jumla ya wanachama, viongozi na watendaji 258,641 walinufaika na mafunzo yaliyotolewa.
Kuhamasisha uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika
Mtendaji huyo amesema Tume kwa kushirikiana na Benki ya CRDB PLC pamoja na Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), imeendelea kuhamasisha na kuratibu uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ambayo itahudumia wanaushirika kupitia Vyama vya Ushirika na wananchi wengine.
“Hadi kufikia Desemba, 2022 mtaji wa KCBL umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 1.7 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni 4.45 mwaka 2022/2023 ikiwa ni asilimia 27 ya mtaji wa Shilingi Bilioni 15 unaotakiwa kufikiwa na benki ili iweze kupewa leseni ya kufanya biashara ya fedha nchini.
Amesema Benki ya Taifa ya Ushirika inatarajiwa kuanzishwa rasmi ifikapo Juni, 2023.
Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika
Amesema katika kuimarisha ukaguzi kwenye vyama vya ushirika, Tume imenunua vitendea kazi ambavyo ni pamoja na magari 12 na pikipiki 146 zilizosambazwa kwenye Halmashauri 146.